WIZARA ya Biashara Viwanda na Masoko imeeleza kuwa itaendelea kuwaelimisha Wafanyabiashara na wananchi kwa jumla juu ya utekelezaji wa sheria mpya ya Biashara ya Zanzibar ya mwaka 2013 ambayo imeweka masharti ya udhibiti wa bidhaa za nguo za ndani kuingizwa na kusafirisha nguo hizo. Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Forodhani, Naibu Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Thuwayba Edington Kisasi amesema Serikali bado haijashindwa kutekeleza sheria hiyo kinyume na ilivyoandikwa na Gazeti moja la kila siku la lugha ya Kiswahili linalochapishwa mjini Dar es salaam. Amesisistiza kwamba si vyema kwa wananchi kutumia nguo za ndani za mitumba kwani ni kweli imethibitishwa na wataalamu kwamba zinasambaza maradhi ya kuambukiza . “Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imebainika kwamba nguo hizo kwa kiasi fulani ni chanzo cha maradhi ya kuambukiza na ndio ikapelekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutunga sheria ili kudhibiti bidhaa hizo,” alisema Naibu Waziri. Ameeleza kuwa kifungu namba 39 (2) cha sheria hiyo kinafafanua zaidi juu ya kudhibiti bidhaa za mitumba ya ainaya nguo za ndani, magodoro na mitumba. Naibu Waziri ameyataja Makampuni makubwa yanayoingiza bidhaa za mitumba nchini kuwa ni Hakuna matata, Damu.com, Bwana Suleiman Mwarabu na 3Savana.com Ltd Amewataka waandishi wa habari kuwa makini wanapoandika habari, hasa wakati huu ambapo kikao cha Baraza la Wawakilishi cha kujadili bajeti ya Serikali kinaendelea, kwa kuandika ukweli na kuacha kupotosha wananchi.