MBOWE ANA KESI YA KUJIBU KATIKA MASHTAKA YA KUMSHAMBULIA MWANGALIZI WA UCHAGUZI MKUU
Freeman Mbowe |
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
ameingia matatani baada ya Mahakama ya Wilaya ya Hai kuona ana kesi ya kujibu katika
mashtaka ya kumshambulia mwangalizi wa ndani katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2010.
Uamuzi huo ulitolewa jana na hakimu
mfawidhi wa wilaya hiyo, Denis Mpelembwa mbele ya Mbowe, wakili wake, Issa
Rajabu na mwendesha mashtaka, Inspekta Marwa Mwita.
Mpelembwa alisema mashahidi saba wa
upande wa mashtaka wameishawishi mahakama kuwa siku hiyo kuna tafrani ambayo ilitokea
na ambayo Mbowe atatakiwa kutoa ufafanuzi wa kuhusika kwake.
Alisema ingawa upande wa utetezi
ukiongozwa na wakili Albert Msando na baadaye Rajabu, ulitoa hoja kuwa ushahidi
wa Jamhuri uliacha mashimo mengi, yeye anaona Mbowe ana kesi ya kujibu.
“Katika hoja zao (utetezi) wanaona
ukiacha ushahidi wa Nassir Yamin, hakuna shahidi mwingine aliyethibitisha
kushuhudia Nassir akipigwa,” alisema akinukuu hoja za mawakili wa utetezi.
Hakimu aliongeza kusema: “Utetezi pia
walitoa hoja kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuwaita akina mama ambao wanadaiwa
kushuhudia, hivyo kuacha mashimo mengi katika ushahidi wao.”
Hata hivyo, hakimu alisema katika hoja
zao ambazo ziliishawishi mahakama, upande wa mashitaka ulijibu kuwa sheria
haiwabani kuleta kila shahidi kujenga msingi wa kesi yao.
“Ni rai yao (mashtaka) kuwa mashahidi wao
saba wameweza kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa pasipo kuacha mashaka ama
mianya kama utetezi walivyodai,” alisema Mpelembwa.
Hakimu Mpelembwa alisema baada ya kupitia
hoja za mawakili wa pande zote mbili, anaona upande wa Jamhuri umeweza kuishawishi
mahakama kuwa mshtakiwa ana kesi ya kujibu.
Kutokana na uamuzi huo, Hakimu alisema
mahakama inampa nafasi Mbowe kujitetea na kesi hiyo imepangwa kutajwa Julai 17,
siku upande wa utetezi utakapotoa orodha ya mashahidi wao.
Katika uchaguzi huo mkuu wa 2010, Mbowe aliibuka mshindi kwa kupata kura 28,585 akifuatiwa na Fuya Kimbita (CCM), kura 23,349, Hawa Kihogo (UDP) 258 na Petro Kisimbo (TLP) 135.