HABARI YA KUSIKITISHA JINSI YULE MTOTO ALIVYOFICHWA UVUNGUNI MWA KITANDA MIAKA 6, KWA KWELI NI MAJONZI
Mashuhuda waliokuwepo wakati wa kufichuliwa kwa mtoto huyo, wakiwemo majirani na wapangaji wa nyumba aliyokuwa akiishi, walisema mpangaji wa chumba hicho, Masumbuko Mkwama (25), aliishi peke yake kwa muda mrefu kabla ya miezi mitatu iliyopita, kuja na mwanamke aliyemzidi umri, Salah Mazengo (36) aliyemtambulisha kama mke wake akiwa na watoto watatu.
Msimamizi wa nyumba hiyo, Donata Sisie ambaye alidai mwenye nyumba anaishi Morogoro mjini, alisema baada ya kumuhoji mwanamke huyo, alisema alikuwa na watoto watano na kila mmoja alikuwa na baba yake na kwamba watatu kati yao, walichukuliwa na wazazi wao na hivyo kubaki na wawili, Elias mwenye umri wa miaka nane na mdogo wa mgongoni.
“Juzi Julai 8, Masumbuko aliwafuata wapangaji wenzake watatu na kuwaeleza kwamba mkewe ana mtoto mlemavu ambaye ni mgonjwa, lakini mwanamke huyo hataki mwanaye atibiwe, jambo ambalo linamshangaza. Kwa pamoja, watu hao walikwenda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kitongoji, ambaye baada ya kuelezwa juu ya mtoto huyo, aliamua kwenda polisi.
“Juzi ulitokea mvutano mkali hapa kwani mama mzazi wa Sala alifika akitaka kuchukuwa vyombo vilivyomo ndani ya chumba cha Masumbuko, mimi nilimzuia kwa hoja kwamba ninachojua chumba ni cha mvulana hivyo nimevichukua vitu vyake na kuvihifadhi kwangu hadi atakapofika.”
Mmoja wa wapangaji wenzake na Masumbuko, Asha Mohamed alisema alipohamia yeye na mumewe, walimkuta Masumbuko akiishi peke yake hadi miezi mitatu iliyopita walipomuona akimleta mwanamke mtu mzima aliyekuwa na watoto watatu, mmoja akiwa na ulemavu wa miguu.
Alisema alimuona mtoto mlemavu akiwa salama kwa siku moja tu, ile aliyofika na tangu hapo hakumuona tena.
“Niwe mkweli kwenye hili, mtoto huyu alifichwa uvunguni tangu ahamie hapa, hii inatokana pengine na ugumu wa maisha kwani kwenye chumba chao wana kitanda futi nne na wanalala wanne baba, mama mtoto wao mkubwa Elias na huyo mtoto wa mgongoni, kuna kipindi nilimuuliza Devota alikuwa wapi aliniambia kuwa alimpeleka kwa bibi yake yaani mama yake anayeishi kitongoji kinachofuata,” alisema Asha.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa kitongoji hicho, Dotto Hambosi alisema baada ya kupewa taarifa na wananchi wake aliwasiliana na polisi, ambao kesho yake walifika na kumkamata mwanamke huyo baada ya kukiri kuwa na mtoto uvunguni mwa kitanda chake. Baadaye walimpeleka Kituo cha Polisi Dumila kabla ya kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa anakopatiwa matibabu.
Juu ya kazi za wazazi hao wawili, Hambosi alisema mwanaume anauza mishikaki na mwanamke pombe za kienyeji katika kilabu cha pombe za kienyeji.