TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU
WABUNGE WA CHADEMA KUONEKANA DODOMA
Kumekuwepo na madai yanayosambazwa kupitia njia mbalimbali za
upashanaji habari kuhusu baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kuonekana mjini Dodoma au kujisajili kwa ajili ya kuhudhuria vikao
vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini humo.
Chama kupitia Idara ya Habari kingependa kutoa ufafanuzi kama
ifuatavyo;
1.
Uamuzi wa kuwataka wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba wanaotokana na CHADEMA kushirikiana na wenzao wanaounda Umoja wa Katiba
ya Wananchi (UKAWA), kutoshiriki vikao vya bunge hilo ili kuepuka kunajisi
mchakato wa Katiba Mpya, ulitokana na maazimio ya kikao cha Kamati Kuu
iliyoketi Julai 18-19 na kuazimia kwamba;
Wajumbe
wa Bunge Maalum wanaotokana na CHADEMA, kama sehemu ya UKAWA, watarudi
kwenye vikao vya Bunge Maalum endapo tu mamlaka ya Bunge hilo
yatafafanuliwa kuwa ni ya kuboresha, na sio kuibomoa au kuifuta, misingi
mikuu (basic features) ya Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya
wananchi na kuandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoteuliwa na
Rais kwa ajili hiyo;
Wajumbe
wa Bunge Maalum wanaotokana na CHADEMA, kama sehemu ya UKAWA, watarudi
kwenye vikao vya Bunge Maalum endapo tu, na baada ya, ufafanuzi
uliotajwa katika aya ya 2 utahusisha marekebisho ya kifungu cha 25 cha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, inayohusu mamlaka ya Bunge
Maalum, pamoja na Kanuni husika za Bunge Maalum;
Wajumbe
wote wa CHADEMA katika Bunge Maalum hawatashiriki katika kikao chochote
cha Bunge Maalum au Kamati zake hadi hapo ufafanuzi wa mamlaka ya Bunge
Maalum uliotajwa katika aya za 2 na 3 utakapofanyika kwa mujibu wa
maazimjo ya Kamati Kuu;
Hadi wakati huu tunapozungumza hakuna jambo
hata moja kati ya hayo lililofanyika, huku mazungumzo yaliyotarajiwa kuokoa
mchakato yakiwa yamevunjika, kwa sababu CCM na Serikali yake wameamua kudharau
na kupuuza maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba badala yake
kuweka maslahi ya chama hicho kwenye katiba.
2.
Iwapo kuna mjumbe/wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba wanaotokana na CHADEMA wameonekana wakijisajili kwa ajili ya kuhudhuria
vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma au watashiriki
vikao vya bunge hilo au kamati zake, wataandikiwa barua ya kujieleza kisha
chama kitachukua hatua kwa mujibu wa taratibu zake.
3.
Tunapenda
pia kuwakumbusha wanachama wa CHADEMA na umma mkubwa wa Watanzania kuwa, mji wa
Dodoma mbali ya kuwa Makao Makuu ya Nchi pia inapatikana Ofisi Kuu ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba ambako
hakujaridhiwa na Watanzania wengi, hakujazuia shughuli za Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kufanyika ikiwemo kutoa huduma kwa watu mbalimbali ikiwa
ni pamoja na wabunge. Suala hilo linakwenda sambamba na ukweli kwamba sehemu
kubwa ya watumishi wa Bunge Maalum la Katiba ni wale wale ambao wanatakiwa
kuwahudumia wabunge wa Bunge Maalum la Katiba.
Hivyo kuonekana kwa mbunge yeyote wa CHADEMA
mjini Dodoma au kwenye viwanja au Ofisi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania hakuwezi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa mbunge husika amehudhuria
vikao vya Bunge Maalum la Katiba, kinyume na msimamo wa UKAWA.
Imetolewa
leo Alhamis Agosti 7, 2014 na;
Tumaini
Makene
Mkuu wa
Idara ya Habari- CHADEMA