CHADEMA KILOSA WABAINI MCHEZO MCHAFU
UONGOZI mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo
la Kilosa mkoani Morogoro umeanza kazi kwa kunasa makada wanne wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Magomeni wilayani hapa wakiwa na nyaraka
za serikali kinyume cha sheria wakiandikisha majina ya watu.
Wakizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CHADEMA wilayani
Kilosa, Seleman Simba na Katibu wa Jimbo la Kilosa Kati, Mussa Ngongi,
kwa nyakati tofauti walisema makada hao wa CCM waliwanasa Septemba 7
mchana wakiendelea na zoezi hilo la uandikiashaji.
“Kisheria zoezi lilipaswa kufanywa na maofisa watendaji wakishirikiana
na wenyeviti wa vitongoji, tofauti na hivyo uongozi wa halmashauri kwa
makusudi umegawa kwa makada wa CCM vitabu vya kuandikisha majina ya
wakazi vitongoji…kwa mtazamo wetu hii inafanyika makusudi kuiandalia
CCM ushindi katika chaguzi zijazo,” alifafanua Ngongi.
Viongozi hao, walisema mbali na zoezi hilo kushitukiwa kwa kupewa
makada wa CCM kuliendesha badala ya watumishi wa serikali,
walilishitukia kutokana na lilivyokuwa likiendeshwa kwa ubaguzi
likiwatenga wenye itikadi tofauti na CCM na wenye misimamo tofauti.
Walibainisha kuwa kilichowashangaza zaidi ni hata baada ya suala hilo
kufikishwa kituo kikubwa cha polisi wilayani hapa, Polisi akiwemo mkuu
wa kituo hicho walilazimisha suala hilo kumalizwa kwa mazungumzo badala
ya sheria kufuta mkondo wake.
Katika ufafanuzi wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Idd
Mshili, mbali na kukiri kuwepo kwa zoezi la utambuzi wa wakazi
unaofanyika kila baada ya miezi mitatu, alikana halmashauri hiyo kutoa
kazi hiyo kwa makada wa CCM zaidi ya maofisa watendaji anaowatambua
kisheria.
Chanzo