VICKY KAMATA ADAKWA NA POLISI KWA KUTUMA UJUMBE WA VITISHO KWA WABUNGE
MBUNGE wa Viti Maalumu, Vicky Kamatta (CCM), amekamtwa na Polisi Mkoa
wa Dodoma kwa tuhuma za kuwatumia ujumbe mfupi wa simu za matusi
wabunge wenzake.
Chanzo ncha kuaminika kutoka mjini Dodoma kiliambia MTANZANIA kuwa
kwa kipindi cha miezi kadhaa Vicky amekuwa akituma sms za matusi kwa
wabunge wenzake wa viti maalumu kupitia CCM, Catherine Magige na Lucy
Mayenga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui.
Taarifa zaidi zinasema kuwa wabunge hao walikuwa wakitumiwa sms za
matusi kwa namba 0653 762 *** ambapo baada ya kuona hali imekuwa ikizidi
waliamua kwenda kufungua jalada la malalamiko katika Kituo Kikuu cha
Kati mjini Dodoma na kuomba ufanyike uchunguzi ili waweze kumbaini
mwenye namba hizo.
Kutokana na maelezo hayo, Jeshi la Polisi lilianza kufanya uchunguzi
kuhusu sakata hilo na kubaini namba hiyo imesajiliwa kwa jina la mdogo
wa kiume wa Vicky.
Baada ya Jeshi la Polisi kufuatilia, ilibainika namba hiyo ilikuwa ya mbunge huyo ingawa hakuisajili kwa jina lake.
Uchunguzi zaidi ukabaini kuwa sms za matusi alizokuwa anatuma, pia
alikuwa akitoa taarifa kwa mwenye namba 0767 500***, akimweleza namna
anavyopambana na wabunge wenzake kwa kuwatukana.
Habari zinapasha kuwa polisi wamekuwa wakifuatilia suala hilo kwa muda licha ya kuwa mara nyingi namba hiyo huwa imezimwa.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa Septemba 28, mwaka huu polisi waliokuwa
wanachunguza suala hilo walifanikiwa kuipiga namba hiyo na kupokewa.
Chanzo cha habari kinaeleza kuwa baada ya namba hiyo kupokewa
aliyepokea aliulizwa ni wapi alipo na kama inawezekana afike kwenye
viwanja vya Bunge kuchukua mzigo wake.
“Aliambiwa hivyo kwa sababu SMS ya kwanza inasemekana kuwa ilitumwa
na mtu aliyekuwa kwenye viwanja vya Bunge, na yule kijana aliyepokea
simu bila kujua aliwaelekeza polisi nyumbani kwao akisema ndipo alipo
mwenye simu.
“Polisi walipofika huko walimtaka kijana aliyekuwa nyumbani apige ile
namba na akapokea yule kijana aliyewaelekeza polisi,” alisema.
Wakiwa wanafanya uchunguzi askari polisi waliipiga simu 0767 500***
ambapo ilipokewa na kigogo mmoja wa ngazi za juu serikalini ambaye baada
ya mahojiano alitakiwa afike kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi.
Kigogo huyo baada ya maelezo alimtaka askari anayefanya upepelezi wa
kesi hiyo kuwa mvumilivu kwani muda ambao alikuwa akihitajika kituoni
isingiwezekana kutokana na kuwa anapiga kura bungeni kuhusu Katiba Mpya.
Chanzo hicho kilisema pamoja na majibu hayo, mpelelezi huyo aliingiwa
na hofu baada ya kutajiwa jina la kigogo huyo wa ngazi za juu
serikalini.
CATHERINE MAGIGE
MTANZANIA ilipomtafuta mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige
(CCM), alikiri kupokea matusi na kufungua kesi katika Kituo Kikuu cha
Polisi Kati mjini Dodoma.
Alisema Septemba 2, mwaka huu alipokea matusi kupitia ujumbe mfupi wa
simu ya mkononi hali iliyomshitua na kuamua kuizima ili isitumiwe tena
kumpigia wala kutuma sms.
Alisema kuwa baada ya kuzungumza na baadhi ya watu walimshauri
kufungua kesi polisi ili uchunguzi ufanyike na anayetuma matusi hayo
akamatwe.
Alieleza kuwa Septemba 3, mwaka huu alikwenda Kituo Kikuu cha Polisi
Kati Dodoma na kufungua jalada la kesi dhidi ya mtu huyo aliyekuwa
akimtukana kwa sms.
“Nilipokuwa pale polisi sasa ndiyo nikaifungulia ile namba na kumbe
kuna sms nyingine zilikuwa zimeshatumwa zikawa zinaingia kwa fujo.
“Ukijaribu kuangalia unaona sms ya kwanza ilitumwa na mtu akiwa
kwenye eneo la viwanja vya Bunge, nyingine Naam Hotel na nyingine maeneo
ya Uwanja wa Ndege hapa hapa Dodoma,” alisema Magige.
Alisema kuwa tangu hapo polisi waliendelea na uchunguzi wa suala hilo na jana alipata taarifa kuwa washukiwa wao wamekamatwa.
“Hii simu inaonekana kazi yake kubwa ilikuwa ni kututukana sisi na
wakati mwingine kuongea na kutuma sms kwa (jina tunalihifadhi), kwa
mfano usiku wa Septemba 28 inaonekana kwamba simu hiyo iliongea kwa
sekunde zaidi ya 1,300 (dakika 21.6), na sijui walikuwa wanaongea nini.
“Kwa kweli mimi hata sielewi tumefika wapi kama viongozi tunaweza kuwa tunatumia simu kutukanana hivi,” alisema.
LUCY MAYENGA
Kwa upande wake Lucy Mayenga, alipoulizwa juu ya suala hilo, alisema
amekuwa akitukanwa kwa njia mbalimbali za mtandao kwa takribani miezi
minne sasa.
Alisema kuwa baadhi ya matusi yalipitishwa kwa watu wake wa karibu jambo ambalo lilimfanya aumie, lakini asijue cha kufanya.
Alisema kuwa Septemba mbili alivyoanzwa kutukanwa Magige, baadhi ya sms zilizokuwa na matusi zilimtaja pia Catherine.
“Sasa tukaongea na Lucy mimi wakati huo sikuwa Dodoma na tukashauriana pia na watu wengine ndipo alipoamua kufungua kesi.
“Nilivyokuwa natukanwa mimi nilikuwa sina muda wa kufuatilia na
niliona ni kama nitu kitapita tu ndiyo maana sikufuatilia, sasa
ilivyohamia kwa Catherine na huko nikawa natajwa na mimi pia, nikaona
hapa sasa imefika mbali,” alisema.
KAULI YA VICKY
Akizungumza tuhuma hizo, Vicky alisema anashangazwa na taarifa za
kukamatwa kwake kwani muda wote yeye alikuwa nyumbani kwake na hakuna
jambo kama hilo.
“Mimi silijui suala hilo… Sijakamatwa na muda huu nipo hapa nyumbani
kwangu na sasa ninajiandaa ili nirudi tena katika vikao vya Bunge,”
alijibu kwa kifupi Vicky.
JESHI LA POLISI
Akizungumza sakata hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David
Misime, awali alisita kidogo na baadaye alisema hakuna taarifa zozote
katika mkoa wake za kukamatwa kwa mbunge huyo huku akitaka kujua taarifa
hizo zimetoka wapi.
“Nani kakwambia masuala hayo… hakuna taarifa kama hizo, hatujamkamata mbunge yeyote usiku huo wa jana,” alisema Kamanda Misime.