Header Ads

Leo ni leo Kipenga cha kampeni kimepulizwa

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva akitangaza kuanza kwa kampeni za vyama vya siasa vilivyosimamisha wagombea wa urais, ubunge na udiwani. Kushoto ni makamu mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid na mkurugenzi wa uchaguzi, Kailima Kombwey.   Picha na Anthony Siame 

 Hatimaye kipenga cha kampeni za uchaguzi mkuu kimepulizwa leo wakati wagombea, vyama na mawakala wao watakapotumia siku zisizopungua 63 kujinadi na kunadi vyama vyao, huku wasomi wakitaka wagombea wajikite katika kueleza ni kwa jinsi gani watarekebisha uchumi, elimu, afya, utawala bora, mapambano dhidi ya ufisadi na amani.
Kuanza kwa kampeni hizo ni hatua ya pili kutoka mwisho ya mchakato  wa Uchaguzi Mkuu kabla ya fainali itakayokuwa Oktoba 25 wakati wananchi watakapopiga kura kuiweka madarakani Serikali ya Awamu ya Tano ambayo rais wake atatangazwa ndani ya siku tatu baada ya upigaji kura.
Hadi sasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijatangaza idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura, ingawa ilikuwa ikieleza kila baada ya kumalizika kwa kazi hiyo kwenye mikoa tofauti kuwa imevuka malengo au iliandikisha kwa mafanikio makubwa.
Kwa mujibu wa makisio ya NEC, jumla ya watu milioni 24 walitazamiwa kujitokeza kujiandikisha kupiga kura.
Makada tisa kutoka vyama vya CCM, ADC Maendeleo, UPDP, Chauma, CCK, NRA, TLP, Tadea na Chadema, ambayo inawakilisha vyama vya NLD, CUF na NCCR-Mageuzi, wamepitishwa kugombea urais
Tangu siasa za vyama vingi zirejeshwe mwaka 1992 na uchaguzi wa kwanza kufanyika mwaka 1995, CCM imekuwa ikishinda chaguzi zote baada ya Rais Benjamin Mkapa kushinda mwaka 1995 na kuongoza kwa miaka 10 na kufuatiwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005.
Uchaguzi wa mwaka huu unafanyika miaka 23 baada ya siasa za vyama vya ushindani kurejeshwa nchini, huku hamasa na ushiriki wa wananchi ukionekana kuzidi kukua na ushindani kuongezeka.
Kinachoongeza chachu kwenye uchaguzi wa mwaka huu ni ushindani mkubwa unaotazamiwa kutoka kwa wapinzani baada ya vyama vinne kuunganisha nguvu kupambana na CCM pamoja na kitendo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhamia upinzani na kupewa fursa ya kugombea urais.
CCM, moja ya vyama vichache barani Afrika ambavyo havijaonja joto ya kukaa nje ya dola, imemsimamisha Dk John Pombe Magufuli.
Hadi jana, CCM ndiyo iliyoweka bayana ratiba ya uzinduzi wa kampeni zake baada ya kueleza kuwa itafanya mkutano mkubwa kesho kwenye viwanja vya Jangwani, huku Chadema ikisema kuwa itatangaza siku yoyote kuanzia leo.
Wakati kipenga cha kampeni kikipulizwa, wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema pamoja na vyama kuwa na ilani zake, ni muhimu wagombea wakajikita katika kueleza ni kwa vipi watakabaliana na tatizo la kuporomoka kwa uchumi, elimu, afya, utawala bora, mapambano dhidi ya ufisadi na amani.
Uchumi
“Lazima uchumi ubadilike, wananchi wanataka kujua nini kitafanyika ili wajitegemee, wajiajiri badala ya kuajiriwa,” alisema mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Frank Tilly alipoulizwa mtazamo wake kuhusu kampeni zinazoanza leo.
Suala la kukuza uchumi pia lilizungumzwa na mkufunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM), Dk Eliamani Sedoyeka, ambaye alisema uchumi na elimu ni mambo ambayo wagombea hawatakiwi kuyaepuka.
Dk Sedoyeka, ambaye anatoka kitivo cha kompyuta na mifumo ya hesabu, alisema ingawa takwimu zinaonyesha kuwa uchumi unakua kila mara, ukuaji huo haujaonekana kwenye maisha ya mwananchi.
“Nataka waseme namna watakavyonyanyua uchumi wa kaya, maisha yao yanaimarikaje ikiwa uchumi unatajwa kukua kila mara,” alisema.
Kadhalika, mhadhiri mwandamizi wa Sheria wa UDSM, Dk  Koti Kamanga  alitaka wanasiasa hao wahakikishe uchumi unaonekana katika maisha ya mwananchi ili hata wakulima ambao ni asilimia 70 ya Watanzania waone huo ukuaji wa uchumi.  “Kila siku tunasema uchumi umekuwa, umekuwa wapi wakati wakulima bado wanaishi katika hali ngumu. Wamenufaika vipi na huo uchumi?,” alihoji.
 Alisema wanadi sera hao wanatakiwa kuzungumzia na kutafuta suluhisho kuhusu mfumuko wa bei kwani kila siku bidhaa zinapanda bei bila mpangilio.
Elimu
Kuhusu elimu, Dk Tilly alizungumzia suala la tafiti za wasomi nchini, akisema wataridhika watakapoona tafiti zao zitafanyiwa kazi na kuleta maendeleo.
Alisema wanasiasa hao waeleze mwelekeo wa elimu ya Chuo Kikuu, maendeleo katika tafiti, uvumbuzi katika gesi na mafuta na teknolojia kwani hayo ndiyo mambo yaliyo katika ulimwengu wa sasa.
Kwa upande wake Dk  Sedoyeka alitaka kampeni hizi zilenge zaidi  katika kuboreshwa kwa elimu ili msomi anapomaliza masomo apate mafanikio kupitia elimu yake.
“Mimi kama mwalimu nataka elimu imsaidie mtu kimaisha, shule zetu ni maskini, familia inapeleka watoto shule ili  ifanikiwe, lakini bado umaskini unabaki pale pale,” alisema.
Maoni hayo yanalingana na ya Dk Kamanga, ambaye alisema jambo analotaka lipewe kipaumbele na wagombea hao wa urais ni kuboreshwa kwa elimu ili msomi anapomaliza masomo apate mafanikio kupitia elimu yake.
 “Mimi kama mwalimu nataka elimu imsaidie mtu kimaisha, shule zetu ni maskini, familia inapeleka watoto shule ili  ifanikiwe lakini bado umaskini unabaki palepale,” alisema.
 Meneja Utafiti na  Uchambuzi wa Sera wa Hakielimu,  Godfrey Bonaventure, aliwataka wagombea wasiliache nyuma suala la elimu kwa sababu elimu yetu imejawa changamoto chekwa, kama mazingira ya kufundishia, sera ya kuandaa wanafunzi na walimu wazuri,  kurejesha hadhi za walimu na kuwapa vijana elimu shindani kimataifa.
 “Kwa sasa ufaulu si tatizo, lakini tuangalie namna ya kutoa elimu ambayo itakidhi mahitaji ya masoko katika teknolojia. Utafiti unaonyesha wanafunzi hawawezi kusoma, lakini ni vyema tukapata  elimu itakayotoa ujuzi” alisema .
 Afya
Mbali na elimu, wasomi hao pia walizungumzia suala la afya wakitaka lipewe kipaumbele. Dk Tilly alisema ni muhimu katika uchaguzi huu watiania wakaahidi watalifanyiaje kazi suala la afya. Alisema ongezeko la magonjwa linatishia afya za wengi.
 “Wengi hawana bima za afya, wakati huo huo magonjwa yanazidi kuwa mengi hali inazidi kuwa mbaya,” alisema.
Kwa upande wake Bonaventure alisema kampeni hizo zizungumzie zaidi mfumo wa afya na namna ya kupunguza, na uhaba wa dawa na madhila katika wodi za leba.
Ufisadi
Mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala wa Chuo Kikuu Huria(OUT)  Hamad Salim alisema ni vyema kama wanaowania urais mwaka huu wakajipanga kuondoa mambo makuu matatu  ambayo ni ujinga, umaskini na maradhi.
 Lakini akasema kubwa kuliko yote ni kuhakikisha wanatoa mbinu za kuumaliza ufisadi.
“Kubwa zaidi wanalotakiwa kulifanyia kazi wagombea hao ni kupambana na ufisadi  ambao umesambaa kwa kiasi kikubwa miongoni mwa Watanzania,” alisema.
Utawala Bora
Akizungumzia suala la utawala bora Bonaventure alisema  wanaowania urais kwa sasa  wanatakiwa kuhakikisha wanasimamia utawala bora ambao unaambatana na uwajibikaji.
 Alisema viongozi wanatakiwa wapimwe kwa uwajibikaji, utumiaji mzuri wa rasilimali za taifa, wayajue matatizo ya watanzania katika maeneo yao.
 Teknolojia
 Idadi kubwa ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa walitaka suala la teknolojia lifanyiwe kazi kwa kina kwani ndicho kiini cha maendeleo katika dunia ya sasa.
Salim alieleza kuwa   rais ajaye aweke vipaumbele kwenye matumizi ya teknolojia kwa wakulima,  namna ambavyo rasilimali zitatumika ili kuleta maendeleo , kuimarisha utawala bora na  kuitangaza Tanzania kimataifa.
Dk Tilly aliungana na Salim na kusema kuwa wanasiasa hao waelekeze nguvu kwenye teknolojia kwa kuimarisha tafiti, uvumbuzi katika gesi na mafuta na kwani hayo ndiyo mambo yaliyo katika ulimwengu wa sasa.

Powered by Blogger.