Header Ads

BOCCO: TUTAPAMBANA KUHAKIKISHA TUNAPATA USHINDI NA KUSONGA MBELE


JOHN-BOCCONahodha na mshambulizi wa timu ya taifa ya Tanzania bara ‘Kilimanjaro Stars’ na klabu ya Azam FC John Bocco ‘Adebayor’ amesema leo watapambana kuhakikisha Kili Stars inasonga mbele kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano ya Challenge Cup inayoendelea nchini Ethiopia.


Kilimanjaro Stars leo itashuka uwanjani kupambana na wenyeji wa michuano hiyo timu ya Ethiopia kwenye mchezo wa robo fainali  wakati Uganda itakuwa ikiumana na Malawi kwenye mchezo wa robo fainali pia.

“Tunamshukuru Mungu tumemaliza mechi zetu za makundi salama na tumeweza kuongoza kundi tunashukuru kwa hilo, lakini pia nawashukuru wachezaji wenzangu kwa kuweza kupambana kwa nguvu kuitetea timu yetu na kuivusha kwenda raundi nyingine”, amesema Bocco kuelekea kwenye mchezo kati ya Kili Stars dhidi ya Ethiopia.

“Tunajipanga kwa mechi hiyo kuweza kushinda na kufuzu kwenda nusu fainali, mechi ya leo ni muhimu na timu yetu inataka kucheza nusu fainali na Mungu akipenda tuweze kufika fainali na kutwaa ubingwa kwahiyo kilichobaki ni kupambana uwanjani”.

“Ethiopia ni nzuri, inawachezaji wazuri wanaopambana lakini naamini katika mchezo wa mpira lazima kuna makosa ambayo wanaweza kufanya na sisi tutatumia vizuri nafasi tutakazozipata ili kupata ushindi”.

“Tunaomba watanzania watuombee na sisi tunapambana tupo kwa ajili ya nchi na tutapambana kwa mioyo yetu yote ili tuweze kupata mafanikio kwenye mashindano haya”.
Powered by Blogger.