Arsene Wenger asema Jack Wilshere atachezea Arsenal maisha yake yote
Arsene Wenger amesema anatumaini kwamba kiungo wa kati Jack Wilshere, ambaye kwa sasa amepelekwa Bournemouth kwa mkopo, atasalia Arsenal maisha yake ya uchezaji.
Wilshere, 24, ambaye huchezea timu ya taifa ya Uingereza, alipelekwa Bournemouth kwa mkopo wa msimu mmoja.
Ni mmoja wa wachezaji waliokua kutoka chuo cha kustawisha wachezaji cha Arsenal na aliwachezea mechi yake ya kwanza 2008 akiwa na miaka 16.
Lakini alicheza mechi tatu pekee katika klabu hiyo msimu uliopita kutokana na majeraha.
"Yeye ni mchezaji stadi sana, hahitajiki kufanya jambo jingine kunionyesha uwezo wake," amesema Wenger.
"Binafsi, natumai atasalia hapa maisha yake yote ya uchezaji."
Wenger amesema walizungumza na mchezaji huyo.
Bournemouth watakutana na West Bromwich Albion Jumamosi na Wilshere anatarajiwa kucheza.