PELLEGRINI ASUSA KUPEANA MKONO NA MOURINHO!
>>NI BAADA KICHAPO CHA CITY 2-1 TOKA CHELSEA, STAMFORD BRIDGE!
MENEJA
wa Manchester City Manuel Pellegrini, Jana mara baada ya Timu yake
kuchapwa Bao 2-1 huko Stamford Bridge na Chelsea kwenye Mechi ya Ligi
Kuu England, alitokomea kwenye Vyumba vya Kubadilishia Jezi bila ya
kupeana mkono na Meneja wa Chelsea Jose Mourinho.
Chelsea walishinda Mechi hiyo kwa Bao la
Dakika ya 90 la Fernando Torres ambalo lilimfanya Mourinho ashangilie
kichizi na kupanda Jukwaa la Watazamaji na kujumuika nao kushangilia.
Baada ya Mechi, kwenye Mahojiano na Wanahabari, Pellegrini alisema: “Sikupeana mikono. Sikutaka kufanya hivyo.”
Hata hivyo, Mourinho aliomba radhi kwa ushangiliaji wake na kudai alikuwa akijaribu kumtafuta Mtoto wake wa Kiume.
Amesema: “Kama wanahisi nimefanya kosa,
naomba radhi. Hii ni shamrashamra ya Bao la Dakika ya mwisho. Yeye
[Pellegrini] amepoteza Mechi Dakika ya mwisho na namwonea huruma kwa
hilo. Katika Nchi nyingine tunapeana mikono kabla ya Mechi, na basi.
Kama alihuzunishwa na kufungwa, ninamwelewa. Na kama amehuzunishwa kwa
kosa langu basi nakubali kosa.”
Mourinho na Pellegrini wana bifu lao
tangu huko Spain ambako Mwaka 2010 Mourinho ndio alimbadili Pellegrini
kama Kocha wa Real Madrid baada ya kuondolewa kwa kushindwa kuipa
Ubingwa Real na kumaliza Nafasi ya Pili nyuma ya Barcelona na Kocha huyo
akajiunga na Malaga.
Wakati huo, Mourinho alibatuka: “Nafasi
ya Pili ni Timu ya Kwanza kufungwa. Kama Real wangenifukuza mimi,
nisingekwenda Malaga! Ningekwenda kwenye Timu kubwa huko Italy au
England!”