PLATINI ATAKA FAINALI KOMBE LA DUNIA 2018 ZIWE TIMU 40!!
>>NI KUPINGA AZMA YA FIFA KUPUNGUZA NCHI ZA ULAYA!
>>FIFA, UEFA ZOTE ZATAKA NCHI ZA AFRIKA, ASIA ZIONGEZWE!!
Michel
Platini anataka Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 ziwe na jumla
ya Nchi 40 na nyongeza ya Nchi hizo ni 2 kila moja kutoka Afrika, Asia
na Marekani huku moja moja ni za kutoka Ulaya na Kanda ya Oceania.
Hivi sasa Fainali za Kombe la Dunia huwa
na jumla ya Timu 32 na Michel Platini, Rais wa UEFA, anataka mabadiliko
hayo yaanze kwenye Fainali za 2018 zitakazochezwa huko Russia.
Msimamo huu wa Platini umekuja mara
baada ya Juzi Rais wa FIFA, Sepp Blatter, kutaka kuzipunguza Nchi za
Ulaya kutoka Nchi 13 kwenye Fainali za Kombe la Dunia na kuziongeza
Nafasi hizo kwa Nchi za Afrika na Asia.
Lakini Platini, ambae anadhaniwa
atasimama kushindana na Blatter kwenye Uchaguzi ujao wa FIFA wa kugombea
Urais, amesema mapendekezo yake ya kuwa na Nchi 40 yataongeza muda wa
kuchezwa Fainali za Kombe la Dunia kwa Siku 3 tu na ni hatua nzuri kwa
kila Mtu.
Platini amesema: “Nakubaliana moja kwa
moja na Blatter kwamba tunahitaji Nchi zaidi kutoka Afrika na Asia.
Lakini badala ya kupunguza Nchi za Ulaya ni bora tuongeze Timu ziwe 40
badala ya 32. Tutaongeza 2 toka Afrika, 2 Asia, 2 Marekani, 1 Oceania na
1 Ulaya.”
Platini amesema Fainali za Kombe la Dunia za Timu 40 zitakuwa na Makundi 8 ya Timu 5 kila moja.
Amedai: “Soka linabadilika…Sasa tuna
Wanachama 209 wa FIFA, sasa kwa nini tupunguze Timu kwenye Fainali za
Kombe la Dunia? Lazima tuongeze, tuwape wengi furaha!”