Header Ads

Balozi Seif ali Idd na Ujumbe wake waendelea na ziara yao nchini Marekani

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia kifaa kipya kabisa cha mawasiliano ya kompyuta Maarufu ipad kwenye kampuni ya Microsoft akishuhudiwa na Waziri wa Biashara Kushoto yake Mh. Nassor Ahmed Mazrui. Kulia yake ni Mtaa lamu wa Kompyuta wa Kampuni ya Maicrosoft Mhandisi Daniel Moloznk na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akibadilishana mawazo na Mawaziri wake aliofuatanao nao katika ziara yao Nchini Marekani. Kushoto yake ni Mh. Nassor Ahmed Mazrui Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko na kulia yake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed.
Balozi Seif akiagana na Naibu Mkurugenzi wa Mfuko wa Kimataifa wa Misaada wa Bill na Melinda Gates Bibi Arlene Mitchell mara baada yha mazungumzo yao katika Ofisi ya Mfuko huo zilizopo kati kati ya Jiji la Seattle. Kati kati yao ni Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mh. Nassor Ahmed Mazrui.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Mfuko wa Kimataifa wa misaada wa Bill na Melinda Gates pamoja na ujumbe aliofuatana nao mara baada ya mazungumzo yao kwenye ofisi ya Mfuko huo Mjini Seattle.
Makamu wa Pili wa Rais wa Znzibar Balozi Seif na Ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kutembelea ofisi ya Kampuni ya Microsoft kati kati ya Mji wa Seattle – Washing Nchini Marekani.
Rais wa Chama cha Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar Bw. Abdulla Abass akimpatia zawadi Maalum za Zanzibar Mkurugenzi Mkuu wa kitengo cha Elimu ya Afya cha Microsoft Bwana Bill Crounse Mjini Seattle.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na ujumbe wake akiangalia baadhi ya kompyuta mpya zilizoingia kwenye soko katika ofisi za Kampuni ya Kimataifa bya Microsoft Mjini Seattle – Washington Nchini Marekani. Picha na Hassan Issa wa –OMPR – ZNZ.

Jamii popote pale Duniani  inaweza kuendelea kuishi kwa amani, furaha na afya iwapo Wananchi wenyewe kwa kuzishirikisha Taasisi na mashirika yaliyowazunguuka watazingatia zaidi umuhimu wa taaluma ya kinga badala ya kusubiri tiba.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa kitengo cha huduma za Afya cha Kampuni ya Kimataifa ya mitandao ya Mawasiliano ya Kompyuta ya Microsoft Bwana Bill Crounse wakati akizungumza na Ujumbe wa Zanzibar unaoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambao uko Nchini Marekani kwa ziara ya wiki moja ya Kiserikali.

Bwana Crounse alisema kwamba jamii kadhaa Duniani hasa katika Nchi zinazoendelea nyingi zikiwamo ndani ya Bara la Afrika zimekuwa zikikabiliwa na magonjwa mbali mbali yanayoibuka kila siku kwa kukosa elimu ya kinga.

Alisema Kampuni ya Microsoft licha ya shughuli zake za kibiashara lakini hivi sasa imeamua kutoa elimu ya kinga katika mataifa mbali Duniani kwa lengo la kupunguza maradhi yanayosababisha vifo ambavyo baadhi yake vinaweza kuwepukia.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa kitengo cha huduma za kinga ya Afya  cha Microsoft alieleza kwamba  Taasisi hiyo katika kukabiliana na wimbi la maradhi imejitolea kutoka elimu ya kinga ya afya kwa  kupitia mitandao ya mawasiliano ya kompyuta.

Bwana Bill Crounse alifahamisha kuwa mpango huo tayari umeshahusisha zaidi ya Mataifa 120 Barari Asia na Afrika akizitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni pamoja na Kenya, Somalia, Msumbiji,Misri na Morocco kwa Afrika na India na Bangladesha kwa Asia.

Akizungumzia taaluma inayotolewa maskulini na Kampuni hiyo Mkurugenzi  wa Afrika wa Microsoft Bwana Louis Onyango Otieno alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake kuwa Taasisi hiyo tayari imeshafungua milango ya kutoa taaluma Barani Afrika kwa kutumia njia ya mitandao.

Bwana Otieno alisema elimu hiyo inayokadiriwa kufikia zaidi ya asilimia 44% imelenga kutolewa kwa  watoto wenye umri wa miaka 15 ili kuwajengea uwezo wa kitaaluma.

Mapema Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Zanzibar Nd. Abdulla Mzee Abdulla aliiomba Kampuni ya Microsoft kuangalia upya mikataba iliyowahi kutiliana saini na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendelea kusaidia sekta ya elimu Zanzibar.

Nd. Abdulla alisema Serikali ya Marekani kupitia Taasisi zake ikiwemo ile ya Microsoft ziliwahi kusaidia kuanzisha mradi wa kuimarisha elimu kwa kutumia mitandao ya kompyuta kwa skuli za msingi Unguja na Pemba.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliipongeza Kampuni hiyo ya Microsoft kwa juhudi zake inazochukuwa za kusaidia taaluma tofauti ikilenga zaidi zile nchi zinazoendelea ikiwemo Zanzibar.

Balozi Seif alisema misaada ya taasisi hiyo kwa kiasi kikubwa imeziwezesha nchi changa kupiga hatua kubwa kielimu na kuiomba Kampuni hiyo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za kuimarisha sekta ya elimu.

Baadaye  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake waliendelea na ziara yao kwa kutembelea Ofisi za Mfuko wa Kimataifa wa misaada wa Bill na Melinda Gates zilizopo kati kati ya mji wa Seattle - Washington.

Katika mazungumzo yao Ofisa Mipango wa Mfuko huo Bibi Windy Wilkins alisema Taasisi hiyo inajaribu kuangalia uwezekano wa namna ya kuisaidia Zanzibar katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu.

Bibi Windy alisema hivi sasa taasisi hiyo kupitia mpango wa AGRA imepanga kuongeza nguvu katika utoaji wa taaluma ya uzalishaji wa maziwa na vifaranga ikilenga kuwajengea  zaidi uwezo wafugaji wadogo wadogo.

Alisema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na wafugaji wengi kuishi vijijini kiasi kwamba taaluma ndio njia pekee itakayowawezesha kuingia katika soko la kimataifa litakalowapa nguvu na uwezo wa kuongeza kipato chao.

“ Kwa kutambua kuwa kilimo ni gari ya Biashara Taasisi yetu imeamua kujipangia kutumia Dola za Kimarekani Milioni mia Nne kwa mwaka katika miradi ya Taaluma “. Alifafanua Bibi Windy Wilkins.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliueleza Uongozi wa Mfuko wa Misaada wa Kimataifa wa Bill na Melinda Gates kwamba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla  muda wote imekuwa ikitilia mkazo sekta ya Kilimo ambayo ndio uti wa mgongo wa Taifa.

Balozi Seif alisema wananchi wengi wa Tanzania na Zanzibar wamekuwa wakiishi katika maeneo ya mashambani kwa zaidi ya asilimia 80% idadi ambayo inapaswa kusaidiwa kitaaluma ili izalishe kitaalamu zaidi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi wa Mfuko wa Kimataifa wa Misaada wa Bill na Melinda Gates kutuma Timu ya wataalamu wa sekta ya kilimo kutembelea Zanzibar ili kuangalia maeneo ambayo wanaweza kusaidia.
Powered by Blogger.