WAMILIKI WA VYUO NA SHULE BINAFSI WAINANGA SERIKALI IMESHINDWA KUBORESHA ELIMU
Mwenyekiti wa wamiliki kanda ya Nyasa, Chelestino Mofuga akitoa tamko |
Mwakilishi wa Wizara ya Elimu Khadija Mchatta akitoa ufafanuzi, |
wamiliki wa taasisi binafsi za elimu kanda ya Nyasa wakisikiliza kwa makini |
Add caption |
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Gerlad Guninita alipokuwa akitoa ufafanuzi wa mipango ya serikali katika kuboresha elimu |
Katika picha ya pamoja |
Katika picha ya pamoja |
WAMILIKI wa shule na vyuo visivyo
vya serikali, wameiponda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakisema haina
mipango dhabiti ya kuboresha elimu nchini.
Wamesema serikali imeshindwa kufanya
maamuzi magumu ya kusimamia ufaulu wa alama 35 na badala yake inaruhusu wanafunzi
wa kidato cha pili na cha nne wanaofeli kuendelea na masomo ya juu.
“Imekuwa kama maigizo ya wasanii
kuhusu alama za ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha pili na nne,” alisema Chelestino
Mofuga ambaye ni Mwenyekiti wa shirikisho la mameneja na wamiliki wa shule na
vyuo hivyo (TAMONGSCO) kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa ya Iringa,Njombe na
Ruvuma.
Katika kikao chao cha siku mbili
kilichofanyika mapema wiki hii mjini Iringa, Mofuga alisema kwa kidato cha pili
TAMONGSCO ilishirikishwa na serikali na mapendekezo yao yalikuwa alama za
ufaulu ziwe kati ya 35 na 40.
“Lakini baadaye serikali ilitangaza
kuwa alama ya ufaulu itabaki kuwa 30 na kwamba nwanafunzi atakayeshindwa
kufikia alama hizo atakariri darasa,” alisema.
Wakati wadau wa elimu wakishangilia
uamuzi huo wa serikali, alisema Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi kupitia barua yake ya Januari 16, mwaka huu, aliwataka wakuu wa shule
zote nchini kuwaruhusu wanafunzi waliopata alama 20 na kuendelea waendelee na
masomo ya kidato cha tatu, mwaka huu.
Mofuga alisema maamuzi hayo
yanawafanya wanafunzi kutokuwa na ari ya kusoma wakiwa na imani kwamba wataruhusiwa
kuendelea na masomo ya juu zaidi hata kama watafeli.
“Maamuzi hayo ya serikali yanachangia
utovu wa nidhamu mashuleni, yanaandaa watazania wasioweza kufikiria vizuri,
kupanga na kusimamia na kutathimini maendeleo ya nchi yao,” alisema.
Alisema maamuzi hayo katika
ulimwengu huu wa utandawazi yanakaribisha ukoloni kwa mlango wa pili kwani
itafika mahali wataalamu wengi wataagizwa kutoka nje.
Akiponda zaidi maamuzi ya wizara,
Mofuga alisema yatawagawa watanzania na kusimika rasmi kundi la watu wachache
wenye uwezo wa kupata elimu bora nje ya nchi kuendelea kuwa bora kuliko watoto
wa wakulima.
Alisema katika ushindani wa soko la
ajira ipo hatari kwa Tanzania kukosa ushindani na nchi za Afrika Mashariki na
nyingine nyingi duniani kwa kukosa ubora wa elimu.
Akifungua mkutano huo, Kaimu Mkuu wa
Mkoa wa Iringa, Gerald Guninita alisema sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 1995
iko katika mchakato wa kufanyiwa marekebisho.
Alisema katika mchakato huo kuna
mambo mengi sana yamerekebishwa ili kuendana na mahitaji ya utoaji wa elimu
bora inayopatikana kwa wote na kwa usawa.
“Rasimu hii kwasasa inaangaliwa na
wadau wengine na tuna imani itasainiwa na waziri muda si mrefu; ninawahakikishia
kwamba sera hii itaondoa changamoto nyingi ambazo mnakabiliana nazo katika
utoaji wa elimu bora,” alisema.