Header Ads

Ahly: Kuitoa Yanga ni bahati tu

YANGA_9208d.jpg
Dar es Salaam na Cairo. Kocha wa Al Ahly, Mohamed Youssef amesifu umakini na nidhamu ya hali juu ya mchezo ilioonyeshwa na wachezaji wa Yanga na kusema ushindi wa timu yake ulikuwa wa 'ngekewa' na si uwezo wa uwanjani.
Al Ahly iliiondoa Yanga kwa penalti 4-3 baada ya mchezo huo kumalizika kwa mabingwa wa Afrika kushinda 1-0 hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa bao 1-1 kutokana na Yanga kushinda bao 1-0 katka mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam.
Katika pambano hilo lililofanyika kwenye Uwanja wa Max jijini Alexandria, mabingwa wa Tanzania, Yanga walicheza kwa umakini katika kujilinda na kushambulia.
Yanga walishambulia wote na kila walipopoteza mpira haraka walirudi golini kwao kujilinda kabla ya kuruhusu bao dakika 71 lililofungwa na Sayed Moawad.
Pia, Yanga mara tatu walipoteza nafasi kushinda mchezo huo wakati wachezaji wake Said Bahanuzi, Oscar Joshua na Mbuyu Twite walipopoteza mikwaju yao ya penalti.
Kocha Youssef alisema mchezo ulikuwa mgumu sana kwetu. Tulitaka kushinda katika muda wa kawaida, lakini haikuwa rahisi kwa sababu hatukuwa makini katika kutumia nafasi.
"Watu wengi walifikiri tutawafunga kirahisi Yanga. Hiyo siyo kweli... ilikuwa timu imara, lakini cha muhimu tumefuzu," Youssef aliuambia mtandao wa Cafonline.
"Bao letu tumelipata kama bahati ya Mungu tu, pia tunashukuru kwa kiwango cha juu cha kipa wetu Sheriff Ekramy aliyeokoa penalti tatu."
Naye kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm alisema makosa waliyoyafanya kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam ndiyo yaliyowagharimu Misri.
Akizungumza na gazeti hili, Pluijm alisema kikosi chake kilikuwa na nafasi kubwa ya kuweka historia ya kuwaondoa Ahly, lakini kushindwa kwao kufunga mabao mengi Dar es Salaam yamewafikisha hapo.
"Tungeshinda kwa mabao matatu tu katika mchezo wa kwanza tungekuwa tumepunguza mzigo katika mchezo huu wa marudiano. Ahly hawakuwa na uwezo wa kutufunga mabao mawili huku kwao kulingana na kikosi walichonacho sasa.
Katika hatua nyingine, baadhi ya makocha wa soka hapa nchini wametoa tathimini yao kuhusiana na mchezo wa marudiano kati ya Yanga na Al Ahly.
Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Dk. Mshindo Msola alisema: "Binafsi nilifurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na Yanga kwani ilibadilika hususani sehemu ya kiungo ambayo iliimarika zaidi tofauti na mechi ya kwanza.
"Unajua katika mchezo wa kwanza nafikiri benchi la ufundi halikufanya kazi yao sawa sawa, lakini jana kazi ilionekana kwani walikaba vizuri nadhani Mkwasa alifanyia kazi ushauri wangu ambao nilimpa kabla ya safari." Aliongeza:"Sehemu waliyokosea ni moja tu katika mabadiliko ambayo kimsingi kama walijua kuna penalti endapo hakutakuwa na mshindi ndani ya dakika 90, hawakuwa na sababu ya kumtoa Kiiza na kumwingiza Said Bahanuzi ambaye hata mechi za ligi tu hapa hachezi."
Naye, Joseph Kanakamfumu alisifu mipango ya Yanga katika mchezo huo, lakini alipinga mabadiliko yaliyofanywa na benchi la ufundi.
"Mpango walioenda nao kule Yanga ulikuwa mzuri walishambulia na kujilinda kitu ambacho kiliwafanya wenyeji wachanganyikiwe. Hata hivyo katika mabadiliko nilitegemea baada ya Ngasa kutoka angeingia mshambuliaji, lakini akaingia Chuji (Athuman Iddi)ambaye hakubadilisha chochote."
Chanzo: Mwananchi
(J M)
Powered by Blogger.