Naibu Waziri wa Mambo ya Nje azindua Airtel Rising Stars International Soccer
Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Dkt. Mahadhi
Juma Maalim (Mb.) amezindua rasmi Kambi Maalum ya Kimataifa ya Mafunzo
ya Mpira wa Miguu kwa vijana wa kike na wa kiume wenye umri chini ya
miaka 17 kutoka nchi 12 za Afrika ikiwemo Tanzania.
Uzinduzi
wa Kambi hiyo umefanyika katika Viwanja vya Azam vilivyopo Chamazi
Jijiji Dar es Salaam tarehe 23 Aprili, 2014 na inadhaminiwa kwa
ushirikiano kati ya Kampuni ya Simu ya Airtel-Tanzania na Klabu ya Mpira
wa Miguu ya Manchester United ya Uingereza.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo Mhe. Dkt. Maalim amesema kuwa, kambi hiyo
inalenga kuwapatia mafunzo maalum vijana hao wadogo ili kuwawezesha kuwa
wachezaji mahiri katika mchezo huo ambao unapendwa na watu wengi
duniani ikiwemo Tanzania.
“Mimi
binafsi kama ilivyo kwa mamilioni ya Watanzania, mpira wa miguu una
nafasi maalum katika mioyo yetu na tunazitambua na kuzipongeza jitihada
zinazofanywa na Kampuni ya Simu ya Airtel kwa ushirikiano na Manchester
United katika kusaidia maendeleo ya mchezo huo hapa Tanzania na sehemu
nyingine za Bara la Afrika. Asanteni sana Airtel na Manchester United”
alishukuru Mhe. Maalim.
Mhe.
Maalim alieleza kuwa, mafunzo hayo ambayo yatasimamiwa na Waalimu
kutoka Shule za Mpira wa Miguu za Timu kubwa ya Manchester United,
yanalenga kuwaandaa vijana hao wadogo na kukuza vipaji vyao katika
mafanikio ya mpira wa miguu Afrika kwani watu wanahitaji kuona mapinduzi
katika mchezo huo na kuondokana na matokeo mabaya katika mashindano ya
kimataifa.
“Ushiriki
wa watoto wetu kwenye mafunzo haya ambayo yatajikita katika kuwajengea
uwezo kiakili, kimwili na kisaikolojia, yatawasaidia kuwa na umoja,
yatawapa kujiaamini na hatimaye kuwawezesha kufanya vizuri katika masomo
yao kutokana na afya njema na pia kuwa wachezaji wa kulipwa Barani
Afrika na duniani hapo baadaye”, alisema Mhe. Maalim.
Mhe.
Maalim aliongeza kuwa, anaona fahari kubwa kama mwakilishi wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuwepo kwenye uzinduzi huo
ikiwa ni katika kuhamasisha Diplomasia ya Michezo ambayo kwa sasa ni
muhimu katika kukuza urafiki, undugu, ushirikiano na uhusiano mzuri kati
ya mtu mmoja mmoja kwa maana ya wachezaji na pia kwa nchi na nchi kama
ilivyo kwa vijana hao ambao wametoka mataifa ya nje 11.
“Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa sasa inahamasisha
Diplomasia ya Michezo ikiwa ni njia mojawapo za kuimarisha mahusiano na
mataifa mengine kupitia michezo. Wizara inaunga mkono jitihada
mbalimbali zinazofanywa na Wizara yenye dhamana ya michezo na Taasisi
nyingine zote za michezo na kitendo cha mimi kuwepo hapa leo ni katika
kuongeza nguvu kwenye jitihada hizo ili nchi yetu iendelee kimichezo,”
alisisitiza Mhe. Maalim.
Awali
akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
Airtel-Tanzania, Bw. Sunil Colaso aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa
kuweka mazingira mazuri ya kuwekeza kwenye michezo.
Nae
Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Bw. Ayoub Nyenzi ambaye alimwakilisha Rais wa Shirikisho hilo,
alimshukuru Naibu Waziri kwa kuzindua Kambi hiyo ambayo ni ya pili kwa
Tanzania baada ya ile ya mwaka 2011. Aidha, aliwaasa vijana hao
kuzingatia mafunzo watakayopewa kwani ndio msingi wa maisha yao hapo
baadaye.
Kwa
upande wao Walimu wa vijana hao kutoka Manchester United Bw. Andrew
Stokes na Bw. Neil Scott walisema kwao ni upendeleo wa pekee kufundisha
vijana hao na kwamba Manchester United imedhamiria kushirikiana na
Tanzania katika masuala ya kuendeleza michezo.
Kambi
hiyo ambayo ipo kwa siku tano itahusisha vijana 74 kutoka mataifa 12 ya
Afrika ikiwemo Tanzania. Jina la nchi na idadi ya vijana kwenye mabano
ni kama ifuatavyo; Tanzania (19), Niger (17), Chad (4), Kenya (4),
Malawi (4), Shelisheli (2) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (6). Nchi
nyingine ni Burkina Faso (4), Congo Brazaville (2), Gabon (4),
Madagascar (2) na Siera Leone (6).
-Mwisho-