Kocha Mkuu wa timu ya Mbeya City, Juma Mwambusi ameshinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa msimu wa 2013/2014. Hafla ya kukabidhi tuzo kwa washindi mbalimbali ilifanyika juzi (Mei 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Mbali ya tuzo hiyo, Kocha Mwambusi ambaye hivi sasa yuko nchini Sudan na timu yake kwenye michuano ya Nile Basin alipata pia zawadi ya kitita cha sh. milioni 7.8. Aliyeshinda tuzo ya kipa bora ni Hussein Shariff wa Mtibwa Sugar aliyepata sh. milioni 5.2 wakati Amisi Tambwe wa Simba aliibuka na tuzo ya mfungaji bora. Tambwe naye alipata sh. milioni 5.2. Mchezaji bora wa VPL kwa msimu wa 2013/2014 ni Kipre Tchetche wa Azam FC aliyejipatia sh. milioni 5.2. Tuzo ya refa bora imetwaliwa na Israel Mujuni aliyezawadiwa sh. milioni 7.8. Yanga iliyoshika nafasi ya pili kwenye ligi na kupata sh. milioni 37, pia ilipata sh. milioni 16 baada ya kushinda tuzo ya timu yenye nidhamu ya hali ya juu. Sh. milioni 21 za mshindi wa nne zilikwenda kwa timu ya Simba. Mabingwa wapya wa VPL, Azam FC walipata sh. milioni 75 wakati Mbeya City ilipata sh. milioni 26 kwa kushika nafasi ya tatu. CREDIT;jaizmelaleo blog