WATU saba wamefikishwa katika Mahakama Mkoa wa Tabora wakikabiliwa na tuhuma za mauaji ya askari polisi wawili wa Kituo cha Polisi Ussoko, Wilaya ya Urambo. Waliofikishwa mahakamani hapo jana ni Fransico Kashinje, Haji Athumani, Abeli Benedicto, Sylivesta Mussa, Sadiki Rushikama, Ramadhani Kassim na Mussa Hatibu. Mbele ya Hakimu Mfawidhi, Issa Magoli, Wakili wa Serikali, Nestory Pascal, alidai Aprili 28 mwaka huu, majira ya usiku, eneo la Ussoke, washitakiwa hao walimuuwa Askari Polisi mwenye namba G3388 PC Shabani Mbua kwa kumpiga risasi. Katika shitaka la pili, inadaiwa siku hiyo watuhumiwa hao pia walimuuwa Askari Polisi G 4602 P.E Iddi Suleiman kwa kumpiga risasi. Washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza shauri hilo. Kesi imeahirishwa hadi Juni 9 mwaka huu itakapotajwa tena.