Hebu tukumbushane!!!Je, ni Kweli Kuna Mbingu na Jehanamu?
SEHEMU YA KWANZA
Naamini
umeshasikia maneno kutoka kwa watu mbalimbali ambao hubeza kuwapo kwa
mbingu au jehanamu. Utasikia watu wakisema, “Nani amewahi kwenda huko
akarudi?” au “Huo ni uwongo tu!” au “Tutajua huko huko siku tukifa.”Je, wewe unadhani kuna mbingu au hakuna? Je, wewe nawe unadhani hakuna watu waliowahi kwenda huko na kurudi?
Choo Nam Thomas ni mwanamke chotara wa Kikorea na Kimarekani ambaye amekutana uso kwa uso na Bwana Yesu, si mara moja au mbili, bali mara nyingi. Yeye anatusimulia habari za kweli kuhusu kuwapo kwa mbingu pamoja na jehanamu.
Ninakusihi ufuatane nami katika simulizi hii ambayo naamini, hadi tutakapofika mwisho wake, utakuwa na simulizi ya kwako iliyo tofauti na ile uliyo nayo sasa: simulizi hii ya kweli kabisa itakujenga, kukuhamasisha, na kukupa mwelekeo; na najua Mungu wa mbinguni, kupitia kwayo, atasema nawe kwa namna ya tofauti kabisa itakayokufanya ujiweke mwenyewe kwenye mizani na kujipima. Nami ninamwomba Yesu Kristo akusaidie kufikia uamuzi sahihi.
Simulizi hii nimeifupisha kwa kuchukua mambo machache yanayozungumzia zaidi habari za mbinguni na jehanamu; mambo ambayo Choo alionyeshwa katika safari zake nyingi alizopelekwa huko. Simulizi hii inapatikana katika kitabu kiitwacho Heaven Is So Real, ambacho kwa Kiswahili kimetafsiriwa kwa jina la Kweli Mbingu Ipo na kinasambazwa na kampuni ya Niim Computers & Graphics (T).
Choo anasema: “Tangu pale Mungu aliponiita kwenye huduma ya kinabii, nimejifunza kuwa waongofu wengi wa kawaida hawaamini. Baadhi yao wanaamini kama mbingu ipo. Wengine hawaonyeshi kujali. Na wengine wao huishi kama kwamba dunia yote ni yao.
Ili kuweza kuwaletea wanadamu ujumbe unaohusu kuwapo kwa mbingu na jehanamu, Bwana Yesu alimpeleka Choo mbinguni mara kumi na saba (17).
Choo anasema kuwa: Nchini Korea, familia yangu kamwe haikujishughulisha kabisa na mambo ya dini. Sikuwahi kusikia habari za Yesu hadi hapo nilipokwenda kanisani. Nilikuwa nimesikia tu kuhusu kanisa na Mungu. Niliamua kuwa Mkristo mwezi Februari 1992.
Mnamo Januari 1994, nilipokea moto wa Roho Mtakatifu nilipokuwa naomba nyumbani. Mwezi mmoja baadaye nilimwona Bwana kanisani. Aliketi madhabahuni. Alikuwa na nywele za hariri, na alivaa joho jeupe mno. Tukio hilo lilidumu kwa takribani dakika tano hivi.
Mwanzoni ndugu na rafiki zangu walikataa ujumbe wangu lakini sasa mambo yamebadilika. Wapendwa wangu wote wameokoka.
Sababu iliyomfanya Yesu anichague mimi kwa kazi hii ya muhimu sijaijua, lakini ninatambua kuwa anataka niwaonye watu wa ulimwengu na makanisani kwamba muda uliobaki kukamilisha kazi yake uko ukingoni!
Tarehe 19 Januari niliamka alfajiri huku mwili wangu ukitetema. Hali hii haikuwahi kunitokea nikiwa nimelala. Lakini tangu usiku wa pasaka mwaka 1995, nilikuwa nikitetema kila niwapo kanisani au ninapoomba peke yangu.
Hali ya kutetema katika uwepo wa Bwana ni jambo la kibiblia. Hii ni aina mojawapo ya mwitikio wa mtu pale awapo uweponi mwa Bwana. Jambo hili lilijitokeza pia kwa nabii Yeremia. Yeye anasema: Kwa habari za manabii. Moyo wangu ndani yangu umevunjika, mifupa yangu yote inatikisika. Nimekuwa kama mtu aliye mlevi, na kama mtu aliyeshindwa na divai; kwa ajili ya BWANA, na kwa ajili ya maneno yake matakatifu. (Yeremia 23:9).
Usiku wa tarehe 19, nilisikia sauti. Niligeuza kichwa changu na kuangalia kule sauti ilikotokea, niliona kitu kinachong’aa – umbo lililovishwa nguo nyeupe. Mng’ao ulioandamana na mgeni huyu asiyejulikana ulikuwa mkali sana hata sikuweza kuuona uso wake. Hata hivyo nilitambua kuwa ni Bwana. [Maelezo yangu mimi Jimmy: Choo hakuweza kumwona Bwana usoni kwa kuwa Mungu katika Biblia alipokuwa akiongea na Musa kwamba: Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi. (Kutoka 33:20). Lakini baada ya mambo yote kufikia mwisho hapa duniani, ndipo wale waliookolewa watamwona Mungu uso kwa uso (1 Yohana 3:2]
Bwana alisema, “Binti yangu, wewe ni mtoto mtiifu mno. Nataka kukupa vipawa maalumu vilivyo vizuri. Kwa vipawa hivi utaweza kunitumikia kwa nguvu sana. Nataka uvifurahie vipawa hivi.”
Januari 20, kati ya saa 9 na saa 10 alfajiri, sauti ya Bwana iliniamsha ghafla na kusema, “Binti yangu, nitakutembelea mara nyingi kabla kazi hii haijafanyika. Hivyo basi, nitakutaka uwe unapumzika wakati wa mchana. Nina mipango mingi maalum kwa ajili yako. Nitakutumia sana. Hata hivyo, itachukua muda kukuandaa kwa kazi niliyokuitia kuifanya. Itakupasa kuandika yale utakayokuwa unayasikia kila ninapokutembelea.” Nilishtuka na kushangaa sana kwamba Bwana angenitembelea mara nyingi!
Siku iliyofuata tena, niliamka ghafla kati ya saa 8 na 9. Bwana alisema nami: “Ninakupa nguvu ambayo utaihitaji kwa kazi niliyokuita kuifanya. Ninakuandaa unitumikie. Mwili wako unatetema kadiri nguvu hiyo inavyomiminika ndani yako.”
Tarehe 2 Februari, Bwana alinitembelea tena na alinishirikisha mambo mengi. Aliniambia, “Binti yangu, ninakwenda kukutumia kwa namna iliyo tofauti. Wengi wa watoto wangu wataonekana kushangazwa. Nina vipawa kwa ajili ya watoto wangu wote. Lakini nitampa kila mmoja vipawa tofauti. Binti, nataka ufurahie kile utakachokwenda kupokea.” [Maelezo yangu mimi Jimmy: Biblia inasema: Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofautiza kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. (1 Wakorintho 12:4-7)]
Mwili mpya
Tarehe 19 na 20 Februari, Bwana alinichukua matembezini kuanzia saa 5 hadi saa 7:08 usiku. Alipokuja aliniambia, “Binti, inanipasa nikuonyeshe mambo fulani.”
Alinyoosha mikono yake kuelekea kwangu. Nilijihisi kuwa mwili wangu unanyanyuliwa kutoka kitandani. Nilianza kulia na kutupa mikono ovyo. Nilishangaa labda ndio kwamba ninakufa!
Baadaye nilijiona niko kwenye ufukwe ambao haukuwa na mtu yeyote. Nilikuwa pamoja na Bwana, huku nikiwa nimevaa joho kama lake. Nilikuwa nina mwili mpya! Nadhani unaweza kupata picha ya namna nilivyoshtuka.
[Maelezo yangu mimi Jimmy:Biblia inasema: Tena kuna miili ya mbinguni na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali. (1 Wakorintho 15:40)]