AJALI YA GARI YAUA BABA NA MWANAYE
Watu
wawili, baba na mwanawe, wamekufa baada ya gari walilokuwa wakisafiria
kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea Ikwiriri kuacha njia na kugonga
kingo ya Mto Kihoi na kupinduka.
Kamanda
wa polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema ajali hiyo ilitokea
juzi saa 5:00 usiku, eneo la Kihoi Ikwiriri na aliwataja waliokufa
katika ajali hiyo kuwa ni Ramadhani Nassoro aliyekuwa dereva na mwanaye
Abuu Ramadhani.
Matei
alisema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi. Alisema katika
ajali hiyo, Samira Nassoro alivunjika mfupa wa paja la kushoto na
alipelekwa Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Kaimu
mganga mkuu wa Kituo cha Afya cha Ikwiriri, Edmund Masele alisema maiti
zimekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya maziko.