IMEGUNDULIKA kwamba Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM) ndiye
mfadhili mkuu na mpanga mikakati mkuu wa kundi linalomfuata Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ambalo limeanzisha chama kipya
cha siasa, Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania).
Kwa wiki kadhaa za hivi karibuni, makundi ya wanachama, washauri na
wapanga mikakati wa Lowassa na Zitto wamekuwa wakikutana katika maeneo
kadhaa jijini Dar es Salaam na kupeana mbinu, lengo kuu likiwa ni jinsi
ya kumega Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika mapande ili
kidhoofike kabla ya uchaguzi mkuu 2015.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, Lowassa amejiaminisha kwamba
ndiye atakayekuwa mgombea urais kupitia CCM. Kazi kubwa anayoona mbele
yake ni kuanza mapema kusambaratisha CHADEMA ili kupunguza upinzani
wakati wa kampeni utakapofika.
Zitto naye, ambaye uanachama wake kwa CHADEMA umebaki kwenye makaratasi
tu, anatajwa kuwa ndiye mwasisi mwenza wa ACT, na amekuwa na uhusiano wa
“kikazi” na Lowassa, hata kabla hajaingia kwenye matata ya wazi na
chama chake, ambacho mwishoni mwa mwaka jana kilimvua vyeo vyake vyote
vya uteuzi ndani ya CHADEMA kwa tuhuma mbalimbali.
Katika hatua mojawapo, chanzo kimoja kilicho karibu na Lowassa kimesema
kwamba mapema mwaka juzi, Zitto alimwendea Lowassa na kumwambia kuwa
mustakabali wake kisiasa ndani ya CHADEMA si mzuri, na kwamba alikuwa
tayari kumsaidia Lowassa kufanikisha malengo yake, lakini kwa sharti
kwamba iwapo mbunge huyo wa Monduli atafanikiwa kupata urais, basi
amteue kuwa Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kauli hiyo kwanza ilimstua Lowassa kwa
sababu ilimuonesha Zitto kama kiongozi asiye mwaminifu, ambaye yupo
tayari kufanya hujuma dhidi ya chama chake, jambo ambalo lilimfanya
Lowassa atilie shaka lengo la ombi hilo.
Jambo la pili lililomshtua Lowassa ni cheo kilichopendekezwa na Zitto,
maana kwa mujibu wa Katiba ya sasa, Waziri Mkuu lazima atokane na
wabunge wa majimbo, na awe kwenye chama chenye wabunge wengi.
Kwa kuwa hoja hiyo ilitolewa katika mazingira ya Katiba ya sasa, na kwa
kuwa haikujulikana wakati ule kama Zitto alikuwa bado ni mwanachama na
kiongozi wa CHADEMA, Lowassa hakuipata nafasi kauli hiyo, lakini amekuwa
anaitumia kujadili sura halisi ya Zitto.
Hata hivyo, taarifa zinasema uhusiano wao umeimarika baada ya Zitto
kuchukuliwa hatua na CHADEMA, huku wapambe wa Lowassa wakipita huku na
kule kusambaza propaganda kuwa CHADEMA bila Zitto inakufa.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema Zitto anatarajiwa kujiunga
rasmi na ACT mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, na timu ya Lowassa
imedhamiria kumfadhili ili kujenga taswira ya mpasuko ndani ya CHADEMA,
na kuipa CHADEMA mpinzani mpya ambaye ataifanya ishindwe kumfuatilia na
kumshambulia Lowassa.
Katika kikao cha mwisho kilichofanyika kati ya timu ya Lowassa na
“Vijana wa Zitto” kilijumuisha baadhi ya wapambe wakuu wa Lowassa wenye
kauli ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM, watu wa karibu kifamilia na
Lowassa na washauri wa karibu wa Zitto, akiwamo Mhadhiri mmoja wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.
Ajenda zao nje nje
Moja ya ajenda zao kuu ni kufadhili na kupandikiza watu ndani ya mfumo
wa CHADEMA ambacho kinaendelea na uchaguzi wa ndani, ili wapate nafasi
za uongozi, wazitumie kupata taarifa na mipango ya chama, na baadaye
wajivue nafasi hizo na kukimbilia ACT, na kuleta msisimko wa kitaifa.
Gazeti hili lina taarifa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa sasa wa
CHADEMA ambao “Vijana wa Zitto” wamekuwa wakiwapigia simu na wakati
mwingine kuwatembelea na kuwashawishi ahadi ya fedha na vyeo ili
wajiondoe CHADEMA.
Baadhi hao ni viongozi wa majimbo na mikoa ambao katika uchaguzi
unaoendelea ndani ya chama hawana uhakika wa kuchaguliwa kutokana na
upinzani mkubwa unaojitokeza baada ya chama kukua na kuvutia wasomi na
wafanyabaishara wenye mvuto katika maneo yao.
Baadhi ya viongozi walioendewa au kupigwa simu wamechukua tahadhari, na wametoa taarifa panapohusika ndani na nje ya chama.
Mbinu mojawapo ambayo imekuwa inatumiwa na “Vijana wa Zitto” kujaribu
kuvunja ngome za CHADEMA ni kuwatangazia viongozi hao kwamba ipo idadi
kubwa ya wabunge wa CHADEMA wanaotarajia kujiunga na ACT. Wanawataja
majina kama njia ya kujenga ushawishi.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi hao wameliambia gazeti hili kuwa wanajua
hizo ni mbinu za kipropaganda. Na baadhi ya wabunge wanaotajwa wamesema
hizo ni mbinu za Zitto kutaka kuwagombanisha na chama chao na
kujitafutia njia mpya kwa kutumia majina yao.
Mmoja wao alisema, “Zitto mwenyewe ameshalikoroga. Sasa hii ni tabia ya
kututaja baadhi yetu, mimi na wenzangu kadhaa tumeshasikia, ni ile ile
roho mbaya ya tukose wote. Kwa kuwa yeye amekosana na chama, anatafuta
watu wa kufa naye.”
Mbali na kupandikiza wagombea nafasi za uongozi na kuvizia viongozi
wanaoogopa joto la uchaguzi ndani ya chama, wamekuwa pia na mbinu ya
kushawishi baadhi ya “wagombea watarajiwa” katika baadhi ya majimbo,
wanaotajwa kuweka nia ya kugombea nafasi za uongozi kupitia CHADEMA.
Makada kadhaa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wamezungumza na gazeti
hili na kutumia kauli zijazofanana. Kwa mfano, makada sita walioweka nia
ya kugombea ubunge katika majimbo kadhaa ya kanda ya Ziwa Mashariki na
Magharibi, wamekiri kwamba kila wanapojadili mkakati huu na “Vijana wa
Zitto,” kila mmoja wa nafasi yake anapewa ahadi ya kupewa pesa zote za
kufanyia kampeni.
Vile vile, baadhi yao wamesema kuwa wanaambiwa kwamba iwapo
watakubaliana na mpango huo wa ACT, moja kwa moja watakuwa wamepitishwa,
maana chama hicho hakina mpango wa kupata wagombea kwa kutumia kura za
maoni.
Taarifa zinasema sehemu ya malengo ya vikao ya Zitto na Lowassa ni kutafuta pesa kwa ajili ya mradi huu.
Zipo taarifa zisizothibitishwa kwamba mwezi uliopita Lowassa aliambatana
na Zitto katika ziara ya kimya kimya ya Mkoa mmoja wa kanda ya Ziwa
ambako anasemekana anataka kujenga ngome nzito ya ACT.
“Ninachojua ni kwamba iwapo ACT itafanikiwa kupunguza makali ya CHADEMA,
Mzee atapita kirahisi, maana kikwazo kikubwa alichonacho hadi sasa
hakipo ndani ya CCM, bali CHADEMA,” alisema mtoa taarifa wetu aliye
karibu na Lowassa, ambaye hakutaka kuthibitisha kama wawili hao
walisafiri pamoja kwenda Kanda ya Ziwa
Chanzo: Tanzania Daima
LOWASSA ADAIWA KUFADHII ACT-TANZANIA; YEYE, ACT WAKANUSHA
Reviewed by
Unknown
on
12:27 AM
Rating:
5