HATARI...MAITI ZA FAMILIA 5 ZAZIKWA KWENYE KABURI MOJA
BIWI la simanzi lilitanda JANA Jumanne katika kijiji cha Kimuchu,
eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu, wakati wa mazishi ya watu watano wa
familia moja waliokufa katika hali ya kutatanisha.
Jamaa za marehemu Paul Magu, 35,
mkewe Lydia Wangui, 35 na watoto wao Allen Muhiu (9), Ryan Ndau (8)
naTiffany Wambui (5) walishindwa kuzuia machozi na baadhi yao kuzirai
wakati wa mazishi hayo.
Kasisi James Kamura wa Kanisa la
Kiangilikana Thika, alitoa mahubiri yaliyogusa wengi huku akiitaka
serikali iwaadhibu waliowaua watoto hao na mama yao.
“Ni jambo lenye uchungu sana kwa
familia kuweza kuvumilia. Ni vigumu kuelewa kilichotendeka kwa sababu
wote wamekufa. Damu ya binadamu haifai kumwagwa kama ya mnyama,” akasema
Kamura.
Magu aligongwa na basi kwenye
barabara ya Thika-Garissa nao mwili wa mkewe uliokuwa na majeraha
ukapatikana karibu na hoteli ya Paradise Lost Resort, Kiambu.
Miili ya watoto wao ilipatikana kichakani siku chache baadaye karibu Tatu City, eneo la Ruiru.
Jumanne, miili ya familia hiyo
ilipelekwa eneo la mazishi kwa magari matatu ya kubebea maiti kisha
ikapelekwa kwenye kaburi la pamoja ambapo ilizikwa.
Waombolezaji kadha walizirai na kuondolewa eneo la mazishi.
“Haiwezekani kwamba mauaji haya
yalitekelezwa na mtu mmoja. Kuna watu walio hai waliohusika na uhalifu
huu wa kikatili na ni lazima serikali ichukue hatua,” akasema Kasisi
Kamura akiongoza ibada ya wafu katika nyumba ya wazazi wa Magu, karibu
na mji wa Thika.
Wakazi walifika kwa wingi kwa ibada
na mazishi ambayo yalihudhuriwa na viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na
Mbunge wa Juja Francis Munyua. Gavana wa Kiambu William Kabogo
aliwakilishwa na msaidizi wake Sammy Onyango.
Kukatiza ibada
Mhubiri alilazimika kukatiza ibada mara kadha na kuomba jamaa waliolemewa na huzuni wasaidiwe.
Wazazi wa mama ya watoto hao,
Francis Ndau na Mary Muthoni na jamaa zao wa karibu kutoka Kaunti ya
Nyandarua walishindwa kusimama wakati wa kuimba kwa kulemewa na majonzi.
Kasisi aliwagusa zaidi waombolezaji
aliposimulia matukio yaliyotangulia kupatikana kwa miili ya watoto hao
siku chache baada ya wazazi wao kufa katika hali ya kutatanisha.
“Mimi binafsi niliomba watoto hao
wapatikane wakiwa hai. Lakini nililia walipopatikana wamekufa. Kwa nini
mtu afanye hivi,” akashangaa.
Kasisi Kamura alisema mauaji hayo yalihusu imani na kuwataka polisi wachunguze kilichotendeka.
“Wakenya wana haki ya kujua
yanachofunza mashirika ya kidini na vitendo vyake na ni jukumu la
serikali kuwaondoa wahubiri wanaopotosha,” akasema.
Aliongeza kuwa wakati umefika kwa
serikali kudhibiti mashirika ya kidini kwa sababu vitendo vya baadhi
yake ni vya kutiliwa shaka.
Aliwataka wafuasi wa makanisa wakatae baadhi ya wahubiri wanaotumia dini kujitajirisha.