CWT Iringa yaunga mkono juhudi za Rais Magufuli kupambana na ubadhirifu
CHAMA cha walimu Tanzania CWT
tawi la Iringa kimesema jitihada zinazofanywa na uongozi wa awamu ya tano ya
rais Dr.John Pombe Magufuli zinapaswa
kuungwa mkono na watanzania wote wenye fikra pevu na nia njema ya maendeleo ya
Taifa.
Zuio la posho kwa watumishi wa
serikali, matumizi holela ya fedha za umma pamoja na kutafuta njia mbadala ya
namna ya kusherekea siku ya Uhuru na maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani, ni
miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwa na tija kwa jamii badala ya manufaa
ya watu binafsi.
Kada ya Ualimu ni miongoni mwa
taaluma ambazo zimekuwa zikilalamikia kukabiliwa na changamoto mbalimbali
yakiwemo mazingira duni duni ya kazi.
Lakini kwa sasa tasnia hii ya
Ualimu inaona uongozi wa awamu ya tano wa rais Dr. John Magufuli ni kama unawapa
nuru ya mafanikio yenye kuchochea kasi ya utendajikazi.
Suala la kuondolewa kwa posho
katika vikao mbalimbali vya watumishi wa Umma, ni miongoni mwa mambo
yanayotajwa kuwa yatachangia kuleta usawa baina yao.
Zawadi Mgongolwa ni
mwenyekiti wa CWT Manispaa ya Iringa anasema njia sahihi ya kuyafikia maendeleo
- ni watanzania kwa pamoja kuuunga mkono uongozi wa awamu ya tano wa rais Dr.
John Magufuli kwa kufanyakazi kwa bidii.
Aidha uongozi huu wa CWT Manispaa
ya Iringa unasema kitendo cha rais kutafuta mbadala wa matumizi ya fedha kwa
ajili ya sherehe ni njia sahihi na yenye tija katika kujenga uchumi wa Taifa.
CWT Manispaa ya Iringa inasema
hatua ya kuupongeza uongozi huo wa awamu ya tano, ni baada ya kuona dalili
njema za utendaji wa kazi – ambao umekunjua nyuso za watanzania walio wengi
hasa walimu, ambao kilio chao kikuu ni maisha duni pamoja na mazingira
yakazi yasiyo rafiki.