Header Ads

KABANGE: HATUTACHUKUWA WACHEZAJI KWA MKOPO


KLABU ya soka ya Kagera Sugar imesema haitapokea mchezaji yeyote kwa mkopo kutoka timu za Simba na Yanga ili kuepuka mzigo.

Kauli hiyo imetolewa na Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Mrage Kabange, alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya kusajili wachezaji wapya pamoja na kuwapokea watakaokuja kwa mkopo.

Kabange alisema wao ni chuo cha mafunzo, ila hawataki kuchukua mchezaji ambaye ameshindikana Simba, Yanga au Azam kuichezea timu yao.

Kabange alisema kikosi chao cha mzunguko wa kwanza ni kizuri na wanakiamini licha ya kwamba kulikuwa na matatizo ya kuchelewa kuanza mazoezi, hivyo timu ikakosa kuelewana vizuri.

“Hadi tunamaliza mzunguko wa kwanza tulikuwa sawa na kufanikiwa kuwa katika nafasi ya tano kwa pointi 20, pamoja na yote hayo tunaweza kuongeza wachezaji wawili tu, kwani tulisajili wachezaji 24 awali,” alisema Kabange.

Alisema watasajili beki na kiungo mmoja, ambapo hivi sasa wapo katika mchakato wa kuangalia mwenye kipaji na hawana mpango wa kutafuta kutoka nje ya nchi, kwani wanataka kuibua vipaji vya wachezaji wa ndani ili wasaidie kuwepo kwa timu nzuri ya taifa na si kila siku wanaocheza nje ndio wanatamba katika ligi ya Tanzania.

Mbali na hilo, kocha huyo alisema wataendelea na falsafa yao ya kuibua vipaji kama ilivyokuwa kwa Themi Felix ‘Mnyama’, ambaye hivi sasa anawatoa jasho washambuliaji wa kimataifa kutokana na jinsi anavyocheza.
Powered by Blogger.