MAMENEJA WA SOKA: TAALUMA HATARI KWA ‘KUMWAGA UNGA!’
ENGLAND: MAMENEJA WAWILI TU WAMEDUMU ZAIDI YA MIAKA 5!
MSIMU HUU LIGI KUU ENGLAND WAWILI NJE, NANI KUFUATIA??
LMA YALIA: “NI AIBU!”
MSIMU
wa Soka wa 2013/14 haujafikia hata nusu huko England lakini tayari
Mameneja 9 toka Madaraja ya Ligi ya juu manne wameshamwaga unga huku
kwenye Ligi Kuu England Martin Jol wa Fulham na Chris Hughton wa Norwich
City wakiwa wamekalia kuti kavu.
Ligi Kuu England Msimu huu tayari
imeshapoteza Mameneja wawili ambao ni Paolo Di Canio aliefukuzwa na
Sunderland hapo Septemba 22 na Ian Holloway alieachia ngazi Crystal
Palace baada maji kumfikia shingoni.
Di Canio alikuwa na Sunderland kuanzia
Machi Mwaka huu na Holloway alidumu chini ya Mwaka mmoja kwenye kazi
yake na Crystal Palace.
Kutodumu kwa mda mrefu kwa Mameneja huko
England kunaelezwa kunatokana na Wamiliki Vilabu na Mashabiki wao
kutaka mafanikio ya haraka pamoja na kuwa na Viongozi wasiokuwa na
subira na hili huwafanya Mameneja watimuliwe kila kukicha.
Huko Blackburn Rovers, Klabu ambayo
inamilikiwa na Wauza Kuku toka India wenye Kampuni ya Venky, wameshakuwa
na Mameneja watano katika Kipindi cha chini ya Miaka miwili na nusu.
Hata Meneja wao wa sasa, Gary Bowyer, yupo kwenye wasiwasi wa kung’oka dakika yeyote ile.
Zipo Klabu nyingi huko England ambazo
Meneja hawezi kudumu kwa Miaka miwili na kama akifikisha hapo basi ni
wazi atajiona amefanikiwa.
Mfano ni Chelsea ambapo tangu Meneja wao
wa sasa, Jose Mourinho, aondoke Mwaka 2007 na kurudi mwanzoni mwa Msimu
huu hapo kati wameshapita Mameneja 7.
Akielezea hali hii, Mkuu wa LMA [League
Managers Association], Chama cha Mameneja wa Ligi, Richard Bevan, ambae
aliwahi kuielezea hali hiyo kama ni aibu, amesema”: “Sielewi jeuri hii
ya kwenye Soka imetokea wapi wakati kwenye Taaluma nyingine
haipo….wasiwasi huu wa kutimuliwa ajira unaharibu taaluma hii!”
Takwimu zilizotolewa na LMA zinaonyesha
muda wa Meneja kudumu kwenye kazi yake ni wastani wa Mwaka 1.84 na
kwenye Ligi Kuu England ni Mwaka 2.81, LIGI 1 ni 1.37 na LIGI 2 ni 2.57.
Kwa Msimu uliopita, kwenye Ligi kwa
Madaraja yote, Mameneja 43 walitimuliwa na 20 walijiuzulu ukilinganisha
na 33 waliofukuzwa na 16 kujiuzulu kwa Msimu wa nyuma yake.
Rekodi ya kutimuliwa kwa Mameneja wengi katika Msimu mmoja ni ile ya 2001/2 ambapo Mameneja 53 walifukuzwa.
Mwezi Machi ndio umetambuliwa kuwa ndio
Mwezi hatari kwa Mameneja kwani hapo ndipo wengi hukosa kazi wakati
Klabu zikihaha kutaka kujinusuru kushushwa Daraja kwa Ligi
zinazomalizika Mwezi Mei.
Kwa sasa ni Mameneja wawili tu ndio
wamedumu kwenye vibarua vyao kwa zaidi ya Miaka mitano na hao ni Arsène
Wenger wa Arsenal na Paul Tisdale wa Exeter City.
Msimu uliopita hali hiyo kidogo ilikuwa
na nafuu kwani walikuwepo Sir Alex Ferguson, David Moyes na Tony Pulis
lakini hao sasa wamestaafu, kubadili Klabu na mwingine kuachia ngazi.