BORA KWA DESEMBA-LIGI KUU ENGLAND: NI PELLEGRINI & SUAREZ!!
BOSI
wa Manchester City Manuel Pellegrini ndie ametajwa kuwa Meneja Bora wa
Ligi Kuu England kwa Desemba pamoja na Straika wa Liverpool Luis Suarez
alietwaa Tuzo hiyo kwa upande wa Wachezaji.
Tuzo hizi hutolewa na Wadhamini wa Ligi Kuu, Barclays.
Pellegrini, Mwenye Miaka 60 na Raia wa
Chile ambae alichukua wadhifa wake mwanzoni mwa Msimu baada ya
kutimuliwa Roberto Mancini, ametwaa Tuzo hii kwa mara ya kwanza baada ya
kuiongoza Man City kutofungwa katika Mechi 7 za Ligi kwa Mwezi Desemba.
Man City walishinda Mechi 6 na kutoka
Sare ya Bao 1-1 na Southampton na miongoni mwa ushindi wao ni dhidi ya
Arsenal na Liverpool.
Pellegrini ametwaa Tuzo ya Desemba kwa
kuwashinda Meneja wa Manchester United David Moyes, wa Chelsea Jose
Mourinho na wa Everton Roberto Martinez.
Kwa Msimu huu wa 2013/14, Mameneja
waliotwaa Tuzo za kila Mwezi tokea Agosti ni Brendan Rodgers, Arsene
Wenger, Mauricio Pochettino na Alan Pardew.
Nae Straika wa Liverpool, Luis Suarez,
ametwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Barclays Ligi Kuu England kwa Mwezi
Desemba baada ya kuweka Rekodi ya kuwa Mchezaji pekee aliefunga Bao 10
katika Ligi Kuu ndani ya Mwezi mmoja.
Suarez alianza Desemba kwa kushindwa
kufunga katika kipigo cha Liverpool cha Bao 3-1 toka kwa Hull City
lakini akapiga Bao 4 wakati wanaifumua Norwich City Bao 5-1 Uwanjani
Anfield na kisha kufnga Bao 2 kila Mechi walipozishinda West Ham,
Tottenham na Cardiff.
Suarez ametwaa Tuzo ya Desemba kwa
kuwabwaga Wachezaji watatu wa Man City, Alvaro Negredo, Vincent Kompany
na Yaya Toure, na pia Ross Barkley wa Everton na Theo Walcott wa
Arsenal.