MAN UNITED: “HAMNA DILI NA NDIO MAANA HATUJATANGAZA!”
LEO
huko England zimezagaa ripoti kuwa Straika wa Manchester United na
England, Wayne Rooney, amesaini Dili mpya ambayo ni rekodi mpya lakini
Mabingwa hao wa England wamesema bado hakijasainiwa kitu.
Magazeti kadhaa huko England Leo
yaliandika kuwa Rooney amesaini Mkataba mpya wa Miaka Minne na Nusu na
atakuwa akilipwa £300,000 kwa Wiki na Man United.
Hata hivyo Man United imekanusha habari
hizo ambazo zimedai Mkataba huo thamani yake ni Pauni Milioni 70 hadi
kufikia Mwaka 2018.
Lakini imeripotiwa kuwa Msemaji wa Man United akikanusha kwa tamko: “Hamna Dili na ndio maana hatujatangaza!”
Inaaminika hadi sasa Mazungumzo kati ya pande mbili yanaendelea vizuri na wakati wowote ule makubaliano yatafikiwa.
Tangu mwishoni mwa Msimu uliopita Rooney
amekuwa akihusishwa na kuihama Man United pale Meneja Mstaafu, Sir Alex
Ferguson, aliposema Rooney ameomba Uhamisho kitu ambacho Rooney
mwenyewe alikikanusha.
Mwanzoni mwa Msimu huu, mara mbili Jose
Mourinho na Chelsea yake walitoa Ofa mbili za kumnunua Rooney lakini
zote zilikataliwa na Man United ambao walisisitiza Mchezaji huyo hauzwi
kwa Bei yeyote ile.
Kufuatia kuthibitika kwa kuondoka
Nahodha wa Man United, Nemanja Vidic, mwishoni mwa Msimu huu na pia
kutojulikana kwa hatima ya Naibu Nahodha Patrice Evra ambae Mkataba wake
unamalizika mwishoni mwa Msimu huu, inatarajiwa Wayne Rooney ndie
atapewa Utepe wa Nahodha wa Mabingwa hao wa England.
Mkataba wa Sasa wa Rooney na Man United unamalizika mwishoni mwa Msimu ujao.