Header Ads

GREDA LA MANISPAA YA IRINGA LAHUJUMIWA, MAMILIONI YADAIWA KUTUMIKA

Mstahiki Meya alipokuwa akikabidhiwa greda hilo, Januari 2012
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya halmashauri ya manispaa ya Iringa zimeeleza kwamba: Greda lililonunuliwa na manispaa hiyo kwa mkopo wa Sh Milioni 581 toka CRDB na kukabidhiwa Januari 4, 2012 limeitia hasara halmashauri hiyo.

Hasara hiyo imeelezwa kutokana hujuma zilizofanywa kwenye greda hilo na baadhi ya watumishi wasioitakia maendeleo halmashauri hiyo.

Kwa kile kilichoelezwa na chanzo chetu, tairi za greda hilo zenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 30 zilivuliwa na kuuzwa katika mazingira yanayotatanisha.

Baada ya kuvuliwa tairi hizo za waya, wajanja hao walivisha tairi nyingine mbovu zisizo na waya ambazo hazikudumu kwa zaidi ya miezi miwili.

Kiongozi Mkuu wa halmashauri hiyo alilazimika kuingilia kati sakata hilo na kuunda tume ya uchunguzi iliyokwenda hadi kwa wasambazaji wa mtambo huo wa kuchonga barabara, Mantrac Tanzania Ltd ili kujua kulikoni.

Taarifa ya Mantrac Tanzania Ltd ilikana kuhusika na hujuma hizo na kutoa uthibitisho unaonesha tairi zilizopasuka kwenye greda hilo zina tofauti  na zile zilizouzwa na greda hilo.

"Sisi hatuwezi kuhusika na hujuma hiyo, tukifanya hivyo tutakuwa tunajihujumu wenyewe kwasababu kampuni yetu ndio wasambazaji wakubwa wa mitambo ya aina hiyo," alisema mmoja wa viongozi wa Mantrac Tanzania Ltd bila kutaja jina.

Hata hivyo alisema kwa kuhofia suala hilo kuichafua kampuni yao walilazimika na wao kufanya uchunguzi wao ili kujua kilichopelekea tairi halisi za greda hilo zikafunguliwa na kufungwa zisizo na kiwango.

Kinachoonekana, tairi halisi zilifunguliwa na kuuzwa na kufungwa sizizo na ubora zilizopasuka muda mfupi baadaye wakati greda hilo likifanya kazi.

Ili kuondokana na aibu hiyo, halmashauri hiyo ililazimika kuidhinisha kiasi kingine cha fedha ili kununua tairi mpya.

Mtandao huu unaendelea na uchunguzi wa taarifa hiyo na itakapokamilika itachapishwa ili kuujuza umma wahusika wakuu wa hujuma hiyo.
Powered by Blogger.