DC wa Kilolo, Gerald Guninita Muuliza swali, Bwana Kitosi wananchi wa kidabaga wakifuatilia Profesa Msolla akipokea kero na kuahidi kuzifanyia kazi WANANCHI wa kijiji cha Kidabaga, wilayani Kilolo mkoani Iringa wamemshitaki mkuu wao wa wilaya, Gerald Guninita kwa Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla. Ameshitakiwa kwa kushindwa kutoa matokeo ya tume aliyodai angeiunda kuchunguza tuhuma za ubadhilifu zilizokuwa zikiwakabili waliokuwa viongozi watendaji wa kata hiyo. Wakati aliyekuwa Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Vicent Gaifalo alikuwa akituhumiwa kwa upotevu wa pembejeo za ruzuku za kilimo zilizotolewa kwa walengwa wa kijiji hicho msimu wa kilimo wa 2012/2013 na matumizi yasioeleweka ya zaidi ya Sh Milioni 10 zilizochangishwa na viongozi wa kata ya Dabaga mwaka 2006 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kata hiyo. Mjadala dhidi ya watendaji hao na hatua zilizochukulia na Mkuu wa Wilaya hiyo baada ya kupelekewa malalamiko hayo, uliibuliwa na mkazi wa kijiji hicho Ayubu Kitosi katika mkutano huo wa Profesa Msolla. Huku akishangiliwa na wananchi wengi waliohudhuria katika mkutano huo, Kitosi alisema baada ya tuhuma hizo kufikishwa kwa mkuu wa wilaya; alitembelea kijiji hicho na kutoa maamuzi ya kushughulikia kero hiyo. “Mkuu wa wilaya aliguswa na malalamiko yetu na katika kuyashughulikia akaahidi kuunda tume ya uchunguzi lakini hadi hii leo hatujapata majibu, na hajawahi kukanyaga kijijini hapa tangu wakati huo,” Kitosi alisema huku akimuomba Profesa Msolla kufuatilia suala hilo. Kwa mujibu wa Kitosi, tume hiyo ilikuwa ianze kazi yake Mei mwaka jana na kukabidhi ripoti yake Septemba, mwaka jana. “Mheshimiwa mbunge miezi tisa imepita toka tuahidiwe kupewa taarifa ya matokeo ya uchunguzi wa tume hiyo; hakuna kinachoendelea na mkuu wa wilaya hajawahi kutembelea tena kijiji chetu hiki,” alisema. Alisema wakati wakiendelea kusubiri matokeo ya tume hiyo, kwa nyakati tofauti mapema mwaka huu, watendaji hao wamehamishwa katika maeneo mengine. Akiahidi kulishughulikia suala hilo, Profesa Msolla aliahidi kumtafuta mkuu huyo wa wilaya ili ajue kulikoni kuhusiana na madai ya wananchi wa kijiji hicho. “Jumapili nitakuwa safarini kuelekea bungeni, lakini naahidi nitaongea naye kwa simu na baadaye nitampelekea taarifa yenu kwa maandishi ili majibu mtakayopata yawe na kumbukumbu,” alisema. Alipotafutwakwa simu yake ya mkononi kuthibitisha madai ya wananchi wa kijiji hicho,Guninita hakupatikana.