Kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Vicent Kawawa(28) ameuawa kwa kupigwa na fimbo na kitu kizito kichwani na mganga wa kienyeji aliyekuwa anamtibu ugonjwa wa akili nyumbani kwake katika kijiji cha Buduba kata ya Nyandekwa wilayani Kahama mkoani Shinyanga. Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha alisema tukio hilo limetokea Agosti 5 mwaka huu saa 12 jioni. Alisema Vicent Kawawa mkazi wa kijiji cha Buduba akiwa nyumbani kwa mganga wa jadi aitwaye Mihayo Isheli akitibiwa ugonjwa wa akili aliuawa kwa kupigwa na fimbo na kitu kizito kichwani na mganga huyo na watu waliokuwepo eneo la tukio na kusababisha kifo chake papo hapo. Kamanda Kamugisha alisema chanzo cha tukio hilo ni kwamba mgonjwa alipandisha kichaa na kuanza kumpiga mganga wa jadi na watu waliokuwa eneo hilona ndipo katika kumtuliza mganga alianza kumpiga akisaidiwa na watu hao ambao idadi yao haijajulikani na kusababisha kifo chake papo hapo. Alisema baada ya tukio hilo mganga Mihayo Isheli alikimbia na familia yake pamoja na watu waliokuwa katika eneo hilo na kamba jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi sambamba na kumtafuta mganga huyo wahusika wengine waliokuwa katika eneo la tukio.