CCM yajimarisha, yateua makatibu 27
Nape Nnauye |
KAMATI Kuu ya Halmashauri
Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeendelea na kikao mjini hapa ambapo moja ya
ajenda za kikao hicho ni kujadili mwenendo mzima wa mchakato wa Katiba mpya.
Pia Kamati hiyo imewateua
makatibu 27 wa wilaya ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo vifo na kustaafu, lakini lengo kuu likiwa kukiimairisha
chama kuanzia ngazi za chini.
Akizungumza jana, Katibu
wa NEC, Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema kikao hicho
kimeanza juzi chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Alisema kikao hicho
kimelazimika kufanyika siku moja na nusu kutokana na kutokamilisha kazi ya
kujadili ajenda mbalimbali ambazo zitatakiwa kupelekwa katika kikao cha NEC
kilichotarajiwa kuketi jana mchana.
Alisema pamoja na kujaza
nafasi hizo za makatibu, pia NEC ilifanya uteuzi wa wagombea wa nafasi za
uenyekiti na ujumbe wa Halmashauri
Kuu (NEC) ambao nafasi zipo wazi baada
ya waliokuwa wakishikilia kufariki dunia.
Aliwataja walioteuliwa
kushika nafasi ya makatibu wa wilaya kuwa ni Omar Mtuwa, Acheni Maulid,
Mohammed Gwama, Amina Imbo, Barnabas Nyerembe, Agnes Mfunya, Raphael Maumba,
Naboth Manyonyi na Hamdani Haji Machano.
Wengine ni Agnes Kasela,
Albert Stima, Nobert Kibaji, Kulwa Omar Milonge, Zitta Malyaga, Hamis Kananda,
Ali Yusuf Salum, Magreth Mtatiro na Tabu Ligwesa Zamalu. Pia wamo Julius
Mbwiga, Rhoda George, Lucy Boniface Shee, Helena Chacha, Mafunda Hamis Ali,
Doris Kimambo, Elizabeth Kasmiry, Shaibu Ally Mtawa na Mariam Yusuf.
Katibu huyo wa Uenezi
alisema kutokana na Kamati Kuu kushindwa kukamilisha kazi yake itaendelea
kukamilisha baadhi ya ajenda. Alizitaja baadhi ya ajenda hizo kuwa ni mchakato
wa Katiba pamoja na hali ya kisiasa
nchini na ajenda ya uteuzi na ya namna ya CCM itakavyojipanga kwa ajili ya
kupata ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa zimejadiliwa pamoja na
utekelezaji wa ahadi walizozitoa wakati wa uchaguzi uliopita.
Alisema katika mchakato wa
Katiba, Kamati Kuu itaangalia kazi yote iliyofanyika, ilipofikia na nini
kifanyike kuendelea mbele.
“Kikao hiki si cha
kumjadili mtu, bali ni kujadili hoja za msingi kwa ajili ya kujenga Taifa,
msisikilize maneno ya mtaani sisi hatuna muda wa kujadili watu bali tunajadili
hoja, siku zote maneno hayaisaidii nchi, tayari Katiba Inayopendekezwa imeisha,
sasa tunaangalia yaliyo mbele,” alisema.
Alisema CCM ni chama
kikubwa ambacho hakina utamaduni wa kujadili watu au nani kasema nini kwani
mchakato umekamilika kwa ushindi mzuri. Alisema wanajadili hoja zitakazolijenga
taifa na kulileta taifa kuwa moja na kuliwezesha kusonga mbele.
Kauli hiyo ya Katibu wa
NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, inamaliza uvumi kwamba, pamoja na mengi
mengine, vikao hivyo vililenga kujadili wana-CCM wanaotajwatajwa kutaka kuwania
urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka kesho.
Hadi sasa CCM ndicho chama pekee ambacho baadhi ya
wanachama wake wameibuka na kutangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu
wa mwakani, huku wengine wakikaririwa kueleza nia akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda.
Wana CCM wengine waliotangaza au kuonesha nia ya
kuwania urais ni January Makamba (Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia), Dk. Hamisi Kigwangalla (Mbunge wa Nzega), Edward Lowassa (Mbunge
wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani), Stephen Wassira (Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Sera na Mahusiano), Bernard Membe (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa), Frederick Sumaye (Waziri Mkuu mstaafu) na Mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja.
Source:Habarileo